SIRI ZA BIBLIA: Katikati ya giza na magumu kuna utajiri na mafanikio yako, usiache fursa, ukamdharau BWANA

Hesabu 14:9 

 *Lakini msimwasi BWANA, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; Uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye BWANA yu pamoja nasi, wala msiwaogope.* 


Hii ni habari ya wana wa Israel ambao Mungu alikuwa amemwamuru Musa kutuma wapelelezi katika nchi ya ahadi ambayo ilijaa maziwa na asali. Lakini waliporejea walileta habari mbaya mkutanoni, licha ya kwamba nchi ilikuwa njema sana lakini walihofia majitu makubwa yaliyokuwa yakiishi katika nchi ya ahadi. 


Lakini Kalebu mwana wa Yefune na Yoshua mwana wa Nuni waliwatia moyo wasiogope maana pamoja na na kwamba yale majitu yalikuwa makubwa lakini waliyaona kama chakula kwa sababu wana Mungu ndani yao. 


Kuna watu wengi leo wanasema wameokoka na wengine wanajisifu kwamba wanampenda Mungu na pia wanamwamini Mungu, lakini ni waoga kuanzisha makazi, kufanya biashara, kuanzisha kampuni au kufungua kanisa, kufanya shughuli za kilimo au hata kufungua huduma za msingi kwa kuhofia watu wenye tabia  za uchawi, umwinyi au ubaguzi wa ukabila. 


Usiache fursa au chakula ukionacho kwa kuhofia majitu marefu (Changamoto). Ukiamini Mungu yuko upande wako, una lipi lingine la kuhofu. Hebu fikiria kati ya wapelelezi 12 ambao ni vichwa vya makabila ni wawili pekee ndiyo waliamini katika uweza wa Mungu, ingawa hao wote walishuhudia kwa macho yao namna ambavyo Mungu alipasua bahari, alivyowalisha mana jangwani na kutenda miujiza mikubwa. Tazama ujasiri wa Kalebu 


"Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara moja tukaimiliki; maana twaweza kushinda bila shaka. 31 Bali wale watu waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi." Hesabu 13:30-31. 


Mpendwa kama mimi na wewe tumekosa ujasiri na maono kama Kalebu mahali palipo na maziwa na asali, na tukawa na hofu ya kutumia fursa kwa kuhofia changamoto za uchawi n.k, ni wazi tutakuwa tumeachagua kumdharau Mungu, ni wazi tunapoteza muda wetu kumwamini Mungu, Imani yetu ni bure mbele zake naye atatudharau wala tusiwe na thamani tena mbele zake. 


"BWANA akamwuliza Musa, Je! Watu hawa watanidharau hata lini? Wasiniamini hata lini?" Hesabu 14:11 


Nina shuhuda nyingi sana juu ya haya. Lakini nitasimulia moja ikupe moyo mpendwa ili uweze kutumia fursa bila hofu pale uipatapo. 


USHUHUDA 

Mwaka jana nikiwa katika safari zangu za kibiashara nilipita Iringa mjini kwa shangazi yangu ambaye alinilea nyumbani kwetu nilipokuwa mdogo. Tulikuwa na muda mrefu hatujaonana, ila namshukuru Mungu amekuwa mwenye familia na mwenye upendo ule ule na Mungu amemuinua amepiga hatua. Alianza kunisimulia jinsi alivyoanza biashara ya mgahawa wa chakula. Anasema wakati mumewe alipoanza kusoma Masters ilibidi achague kuacha kazi yake ya kwanza na ndipo mambo yalianza kuwa magumu, akafikiri sana na kugundua fursa pekee ni yeye kutumia kipaji chake cha jikoni yaani kupika. Akawa akipita kila mahali kutafuta eneo la biashara lakini fremu zilikuwa hazishikiki ni wakati huo barabara ya lami ilianza kupita maeneo ya mkwawa kwa sababu ya kuhamishwa kwa ofis ya mkuu wa wilaya manispaa ya Iringa. 


Alipita mahali akakuta kuna fremu zimefungwa, na zimepigwa na vumbi haswaa hadi zimeanza kuchakaa, akapatazama na kuulizia wengi wakamwambia hilo eneo halina biashara watu hukimbia na kufunga. Lakini ndipo palikuwa na unafuu wa bei, maadamu palikuwa barabarani yeye binafsi akaridhika. Akaanza kuuza chapati, chai na supu majira ya asubuhi, ugali na wali mchana. Madereva pikipiki na bajaji wachache waliokuwa wanapita na kuanza kula walisifia mno chakula chake kila mmoja akaanza kuwa balozi kwa kifupi shangazi alikuwa mpishi bora na msafi kuliko mazingira yote ya mama ntilie hatimaye hapo pakawa kijiwe ofisi ikawa kubwa mno kiasi kwamba ilibidi aajiri mabinti wasipongua wanne wamsaidie kazi.


Mwenye eneo akaanza kuona wivu na kumletea visa. Mwanzo alianza kumshutumu kwamba anatumia uchawi kufanya biashara na mwisho alimfukuza pale na yeye akafungua biashara ile ile aliyokuwa ameanzisha shangazi, baada ya mwezi pakarudi katika ile hali ya mwanzo, hakuna kijiwe na fremu zilianza kupigwa vumbi. Wala shangazi hakuwa na siri nyingine ya mafanikio zaidi ya ujuzi wake mkubwa jikoni na kumuomba sana Mungu, hata nyumba yake ipo hivyo siku zote husoma neno la Mungu pamoja, wakitafakari kila mmoja na kufanya maombi kabla ya kulala. Hivyo alipohamisha biashara, akahama na wateja wake. Kwa sababu watu wanapenda kwanza kilicho bora na si mahali ulipo. 


Unafikiri shangazi angekuwa na mawazo yale ya kwamba mahali pale ni pagumu angefanya biashara? Inawezekana Mungu alikuwa anasubiri mwanae mwaminifu kama yeye mwenye ujasiri ili adhihirishe nguvu na uweza wake. Ukiwa mwenye maamuzi na jasiri kama wale wakoma wanne Mungu ataanza kukanyaga na wewe kwenye kila hatua yako.


Shuhuda ni nyingi sana. Lakini chaguo ni lako leo, kufaidi maziwa na asali katikati ya giza na majitu marefu ukiamini Bwana atakushindia au KUDHARAU uweza wa MUNGU. 


Paulo anasema "Basi, tuseme nini juu ya hayo? Mungu akiwa upande wetu ni nani aliye juu yetu." Rumi 8:31 


Katika Wafilipi anadhirisha na kusema.. "Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu." 


Kama alivyosema Kalebu wale watu ni kama chakula, na zifanye leo changamoto za maeneo yenye fursa kuwa kama chakula hakika utafanikiwa. Haijalishi yupo mchaga, mkinga, mhehe, mpogoro, msambaa, mchina, mturuki n.k maadamu Roho wa Bwana amekupa macho ya kuona pesa na ushindi piga kazi, weka bidii katika kuomba. Utapokea ushindi wako. 


Giza, uchawi, umwinyi na nguvu zote za yule adui katika ulimwengu huu havina nafasi mbele ya uso wa Bwana. Msikie Mungu mwenyewe asemavyo.


2 Mambo ya Nyakati 16:9 

Kwa maana macho ya BWANA hukimbia kimbia duniani kote, ili ajionesha kuwa mwenye nguvu kwa ajili ya hao, waliokamilika moyo kuelekea kwake..." 


Unasubiri nini sasa? 


Kapinga Jr 

0718143834

Kapingaemanuel@gmail.com 

Makabe, DSM

Comments

  1. Ahsante sana Kwa kututafakarisha mchana huu na
    hiki Chakula cha kiroho.Ubarikiwe sana Brother

    ReplyDelete

Post a Comment