Euro 140 milioni za Man united kwa Naemar na tuzo ya ballon d’or


Naukumbuka msimu ule wa 2007/2008 wakati manchester united ikiwa kwenye ubora wake, wakati huo Manchester united ikiwa chini ya sir Alex Ferguson iliweza kuzoa mataji maatu lile la ligi kuu uingereza, kombe la FA na klabu bingwa Ulaya, wingi wa mashabiki wa upinzani kuipinga united katika maeneo ya maeneo ya kuoneshea mpira hii ilidhihirisha ni jinsi gani man united ilikuwa bora.

Huo ulikuwa wakati ambao Christian Ronaldo aliweza kutwaa tuzo ya mchezaji bora ulaya na mchezaji bora wa dunia nyuma ya Lionel Messi ambaye ndiye alikuwa ameanza kuwa kwenye ubora wake, Ronaldo alijiunga na Real Madrid akiwa bora na bila shaka aliweza kukubali kujiunga na Real Madrid kwa kuwa ilikuwa bora.

Tangu kustaafu kwa mkongwe sir Alex Ferguson bado united imeshindwa kurejea kwenye ubora wake, David Moyes ambaye ndiye aliyekuwa chaguo la sir Alex Ferguson aliweza kudumu kwa miezi nane na kuinyima timu hiyo fursa ya kushiriki michuano ya mabingwa ulaya na baadae alikabidhiwa kocha Louis Van Gaal ambaye naye hajairejesha timu hiyo kwenye ubora wake.

Louis Van Gaal amekuja na wazo jipya la kumsajili nyota wa Brazil Neymar Jr ambaye anafanya vizuri kwenye timu ya Barcelona akishirikiana vizuri na Lionel Messi pamoja na Luis Suarez ambaye anatisha kwa kutikisa nyavu kwa wapinzani wake, Neymar amekuwa kwenye wakati mzuri katika timu ya Barcelona na aliweza kuingia kwenye  tatu bora ya kinyang’anyiro cha kutafuta mchezaji bora wa dunia.

Pamoja na tetesi kuwa Manchester united imetengenga euro 140 milioni za kumsajili nyota huyo binafsi naona ni ndoto za mchana ambazo hazina mafanikio. Kwa sasa timu za Hispania zimekuwa bora ilikinganishwa na zile za Uingereza ukianza na Barcelona na Real Madrid ambao ni miamba wa La liga, Atletico Madrid pia chini ya Simeon imekuwa kwenye wakati mzuri bila kuisahau Sevilla ambao wanatisha kwenye michuano ya europa.

Manchester united ilishindwa kuvuka kuelekea katika hatua ya 16 bora katika michuano mabingwa ulaya  baada ya kukubali kipigo kutoka kwa Wolfsburg na hatimaye kutupwa katika michuano ya europa. wachezaji wengi bora lazima wafanye vizuri kwenye ligi zao, na mashindano mengine, kama ilivyokuwa kwa Lionel Messi ambaye alikusanya mataji yote muhimu na kuibuka bora msimu huu.

Kama Neymar anataka kuwa bora kama Messi ni wazi kuwa united watakuwa wanatwanga maji kwenye kinu kwa kutoa ofa hiyo, jibu liko wazi kwa sasa huwezi kuwa bora duniani ukiwa na Machester united, ingawa Manchester united ni timu kubwa duniani lakini inahitaji kurudi kwenye ubora wake kwanza ndipo ianze kuhangaika na wakina Neymar ambao wanaweza kuibuka bora kama timu hiyo itarudi kwenye ule ubora wake.

Real Madrid, Barcelona na Bayern Munich zinaweza kusajili nyota wa kubwa na kuipiku Manchester united kwasababu zipo kwenye ubora na ndizo  zinazofanya vizuri katika michuano ya ndani na kabu bingwa ulaya hivyo kuna njia ya mafanikio kwa wachezaji bora wa timu hizo kuliko ilivyo kwa united, wakati huu ambao Edwood Ward na Louis Van Gaal wapo kwenye harakati za kuikomboa timu hiyo.

Ikumbukwe Barcelona ndiyo timu inayoongoza kutoa kutoa wachezaji bora duniani, hayo ni matumaini tosha kwa Neymar ambaye ana imani siku moja atakua bora ilivyokuwa kwa lionel kulingana na kiwango chake kuwa bora wakati wote. Ikumbukwe Ronaldinho Gaucho alikuwa bora wakati lionel messi anachipukia, Neymar 23, yuko nyuma kwa miaka mitano dhidi ya Messi ambaye umri wake ni miaka 28, matumaini yake ni kuwa mtawala wa pale Catalunya baada ya kuondoka kwa ufalme wa Messi na wala si suarez ambaye ana umri sawa na lionel Messi.

Ndiyo maana nilinza kwa kuikumbuka Manchester united ambayo ilimuinua Ronaldo kuwa bora wakati ule wa Ferguson bila shaka alistahili kuchukua tuzo akiwa kwenye timu bora ambayo ilikuwa inaundwa na wachezaji bora. Wakati ule Ronaldo anavunja rekodi ya usajili kwa dau la pauni million 80 bila shaka halikuwa dau pekee lililoweza kumshawishi kutua Santiago Bernabeu bali ni sifa na ubora wa ambao timu ya Madrid ilikuwa nayo na ndiyo maana akiwa na timu hiyo ameweza kuweka na kuvunja rekodi mbalimbali na kuongeza tuzo mbili za kuwa bora duniani.

Kama hali haiko shwari pale Old Trafford ni vigumu Neymar kutua Man united, pamoja na kiasi kikubwa walichotenga hakitaweza kumfanya Neymar kuwa bora duniani. Diego Simeon ambaye ni kocha wa Atletico Madrid aliwahi kunukuliwa akimwambia aliyekuwa kocha real Madrid Carlo Ancelloti hatomfunga tena kama amemwachia Di Maria atimke kwenda united.

Diego Simeon anakumbuka vema kazi ya Di Maria ambayo ilimpokonya taji la klabu bingwa mdomoni, licha ya kutua kwa mashetani hao Angel Di Maria akiwa kwenye kiwango bora alishindwa kufanya vizuri akiwa Luis Van Gaal pale Man united hilo ni tatizo lingine ambalo linaweza kumtisha Neymar ambaye ana matarajio ya kuwa nyota zaidi katika soka, ambaye anafikiria kuwa mwenye mafanikio kama Lionel Messi aingie kwenye kumbukumbu ya vitabu vya wachezaji nguli wa soka duniani

Binafsi naziona euro 140 milioni haziwezi kufanya kazi ya kumleta Neymar pale old trafford labda ubora ule wa Manchester united katika ule msimu wa 2007/08 ambao ulimpa tuzo Christian Ronaldo kwa mara ya kwanza ndiyo unaoweza kumleta Neymar Man united kwa sababu atakuwa na imani ya kuwa bora akiwa na timu iliyo bora na heshima ile ambayo ilijiwekea dunani.      

Comments