Yanga na simba zinavyoleta sura mpya ya usajili Tanzania


 

Naukumbuka ubora wa Nemanja, Naukumbuka na ule ubora wa Branslav Ivanovic ambao wote walitamba na kufanya vizuri wakiwa katika ligi ya Uingereza licha ya kucheza timu tofauti lakini bila shaka Wasebia hao walikua gumzo kutokana na kuwa wagumu kupitika katika safu ya ulinzi, namkumbuka  Rio Ferdinand alivyoishi maisha rahisi pale Manchester united chini ya ulinzi mkali wa Nemanja Vidic, licha ya kusajiliwa kama mlinzi wa kati katika timu ya Chelsea Branslav Ivanovic aliweza kuwa bora kwa kucheza kama mlinzi wa kulia na beki wa kati pale inapobidi kumsaidia John Terry au Ricardo Carvalho, na hadi sasa bado anaishikilia namba pale Stamford Bridge.

Uzuri wa mabeki hao ulizifanya timu za Uingereza  kugeuza macho na kuelekea ulaya mashariki kunako nchi ya Serbia ili kupata walinzi bora ambapo usajili wa mabeki na viungo imara wa kukaba kwa wachezaji kama Nemannja Matic ulifatia.

Naliona hili katika klabu za Tanzania hasa Simba na Yanga, hapa naizungumzia ardhi ya Robert Mugabe ambayo imetuletea mshambuliaji bora katika klabu  yanga Donald Ngoma, kiungo bora Thabani Kamusoko na Yule aliyesajiliwa na simba Justice Majabvi. Wote hawa wajihakikishia namba za kudumu katika timu zao kutokana na kufanya vizuri.

Nikimwangalia Donald Ngoma natamani angekuwa mtanzania ili stars yetu ifike mbali kwa kuwa na wachezaji bora ambao wanaweza kubeba majukumu uwanjani, licha ya kucheza nyuma ya mshambuliaji Amis Tambwe lakini bado Ngoma anazidi kuwa bora, huyu jamaa ana uwezo wa kuendesha timu, kufunga na kutoa pasi za magoli kwa mshambuliaji wake, ni msumbufu na huwaweka walinzi katika wakati mgumu muda wote awapo uwanjani.

Nakumbuka katika ya kombe la mapinduzi baada ya Ngoma kufanyiwa mabadiliko dhidi ya URA ya Uganda, URA ilipata matumaini mapya ya kushambulia kwa kuwa waliamini ni aliyetoka alikuwa tishio kutokana na uwezo wake wa hali ya juu na kasi aliyonayo uwanjani hivyo hawakuwa na hofu iliyowafanya wasipandishe mashambulizi. Mpaka  sasa Donald Ngoma ameifungia yanga magoli 9 katika mechi  15 za VPL alizocheza.

 Namwangalia kiungo huyu mtulivu aliyewafanya makocha na viongozi wa Yanga wamfungie Kiungo Haruna Niyonzima  maarufu kama Fabrigas bila hofu licha ya umahiri wake mkubwa wa kupiga pasi uwanjani lakini kiungo Thabani Kamusoko alidhihirisha jeuri ya timu hiyo kwamba wanaweza kufanya vizuri bila Haruna Niyonzima ambaye hivi karibuni aliomba msamaha kwa timu yake.

Thabani Kamusoko ni kiungo bora ambaye anaweza kuituliza timu, kupiga pasi, kuongoza mashambulizi na uwezo wa kufunga magoli, anapenda kucheza mpira amekuwa shida kwa viungo wa timu za upinzani na kudhirisha kuwa yeye ni mkali ameiwezesha timu yake kukusanya pointi 39 ikiwa kileleni mwa ligi bila uwepo wa kiungo tegemezi Haruna Niyonzima.

Ukirejea katika ule mtaa wa msimbazi bila shaka utamkuta Justice Majabvi ambaye alisajiliwa kutoka uko kwenye ardhi walikotoka wakina Dornald ngoma na Thabani Ngoma, tofauti ni timu walizocheza. Kiungo uyo ana uwezo mkubwa wa kukaba na mtulivu katika kucheza mpira katikati, amekuwa muhimu kwa kikosi cha msimbazi,  Justice Majabvi ana uwezo  wa kucheza kama kiungo mkabaji na beki wa kati na alicheza mara kadhaa kwenye nafasi hiyo akiwa na timu yake ya simba.

Naipenda ile timu yangu ya Ukraine maarufu kama Shakhtar Donetsk ambayo imekuwa ikisajali wachezaji wengi kutoka nchini Brazil ambao wamekuwa msaada mkubwa kwenye ligi yao ya nyumbani na kufanya vizuri katika mashindano ya klabu bingwa na yale ya Europa. Shakhtar wamegundua wachezaji hao wana msaada mkubwa kwao na ndiyo maana Brazil imekuwa shimo lao kubwa la usajili kuliko wachezaji wa nchi za ulaya, ambapo wameweza kuwauza wachezaji ambao ni nyota Luiz Adriano ambaye sasa ni mashambbuliaji wa Ac Milan alimfukuza Christian Ronaldo kwa magoli kwenye michuano ya klabu bingwa ulaya msimu uliopita na Willian da Silva ambaye anang’aa na Chelsea.

Nina mashaka pengine macho ya usajili ya timu zetu za Simba na Yanga hapa Tanzania kuelekea katika ardhi ya Robert Mugabe kwa ajili ya kusaka nyota ambao wataleta ushindani kitaifa na kimataifa , kama wanafanya vizuri kama tunavyoona kutoka kwa kina Ngoma, Kamusoko na Majabvi itakuwa rahisi kwa timu zetu kusajili kutoka Zimbabwe kama ilivyo kwa Shakhtar Donetsk kutoka Brazil. Pengine tutahama Kenya na Uganda na macho ya usajili yatalenga zaidi katika nchi ya Zimbwabwe ambayo nyota wake watatu wameweza kuitangaza nchi yao hapa Tanzania.

 




Comments