Benteke kubaki au kuondoka liverpool?


Kilikuwa ni kipindi kigumu kwa liverpool baada ya kuondoka kwa mshambuliaji wao Luis Suarez kuelekea Barcelona ni wakati huu ambao liverpool ilikuwa ikihaha kupata mfungaji mwingine baada ya Daniel Sturridge kuanza kupatwa na majeraha ya mara kwa mara.

Brendan Rodgers aliamua kumchukua mshambuliaji wa zamani wa manchester city Mario Balotteli aliyekuwa akikipiga katika timu ya Ac Milan lakini alichemsha muda mfupi tangu ajiunge na wekundu hao wa Merseyside na kufunga goli 1 katika ligi ya Epl kwa kipindi chote alichokuwa anfield.

Katika kipindi cha majira ya joto kabla ya kuanza kwa msimu wa mwaka 2015/16 Brendan Rodgers alimsajili mshambuliaji wa Aston Villa Christian Benteke kwa dau la paundi 32 milioni. Jambo hilo liliwashangaza baadhi ya wachambuzi na wahariri wa michezo kutoka katika vyombo vya habari vya Uingereza wengi wakiamini kuwa Benteke hatafiti katika mfumo na aina ya mchezo ambao liverpool inacheza.

Daniel Taylor ambaye ni mwandishi wa michezo wa gazeti Guardin la nchini Uingereza aliwahi kuandika kuhusu Benteke ambaye alisema "Villa inapiga krosi nyingi kuliko klabu nyingine kwenye ligi, hali hiyo hunifanya nifunge mara nyingi".

Benteke amewahi kusema hana hofu ya kutua liverpool, kama liverpool inamwitaji basi bila shaka Brendan Rodgers anafahamu ni namna gani atamtumia. Hata mimi namuunga mkono katika hilo hii ilikuwa si kazi yake kwanza ilikua ni kazi ya kocha Brendan Rodgers ambaye yeye alitakiwa afanye mipango ajue ni namna gani angemtumia.

Ukweli ni kuwa Brendan Rodger hakuwa ameandaa mipango ya kumtumia mshambuliaji huyo ambaye alitengwa na mfumo wake 4-3-3 ambao ulishindwa kufanya kazi. Hii ni kwa sababu 4-3-3 inahitaji washambuliaji watatu ambao wanashirikiana vema kama ilivyo pale Barcelona

Jambo la pili ni kutokana na washambuliaji wa pembeni wa liverpool kuwa na kasi ya kushambulia zaidi kuliko benteke ambaye ameshindwa kuendana na kasi yao. Hii inaonesha wazi kama Sturridge angekuwa hapatwi na majeraha ya mara kwa mara kulikuwa hakuna haja ya kununuliwa kwa Benteke.

Ujio wa kocha Jurgen Klopp bado umedhihirisha kuwa Benteke si aina ya mshambuliaji ambaye anamwitaji na katika kipindi hiki ambacho Sturridge amekuwa kwenye majeraha amekuwa akimtumia Roberto Firmino ambaye ameweza kuendana na kasi yake na amekuwa kwenye wakati mzuri wa kucheka na nyavu kuliko Benteke.

Liverpool ya Brendan Rodgers haikuundwa kushambulia kwa kupiga krosi, kucheza kwa spidi ya kumsubiri Benteke afike kwenye eneo la tukio ili afunge wakati huu wote Benteke alitakiwa kuwa na kitu cha ziada kwa kujituma zaidi awe anapambana bila kusubiri mipira katika eneo la mbele na hii ilimfanya atengwe wakati wote.

Klopp anaamini katika soka la pasi fupi, na kushambulia kwa kasi kama ilivyokuwa pale Dortmund kwa wale waliokuwa wanaifatilia timu hiyo, kwa staili ya benteke bado anashindwa kuendana na kasi yake na hivyo ameaumua kumtumia Firmino. Benteke anahitaji kupigana ili acheze katika timu ya Klopp vinginevyo atafute mlango wa kuondokea.

Mahesabu ya kocha Jurgen Klopp kusajili mshambuliaji mwingine ambaye ataendana na kasi ya timu yake katika kushambulia. Klopp anamtolea macho Jamie Vardy wa Leicester au Mauro Icardi wa Intermilan akiamini atakua na liverpool bora kupitia hao chini ya fundi Felipe Coutinho.

Ingawa Klopp hajaweka wazi kuhusu Benteke nadhani anampa nafasi ya kujifunza namna ya kucheza kwenye timu yake lakini nadhani Benteke anahitaji kuondoka ili kurejesha heshima yake na kupata nafasi katika timu yake taifa nchini Ubeligiji.

Comments