Ni kweli Mourinho atatua Old Trafford?


Inawezekana bado wapenzi wa soka na mashabiki wengi wa Manchester united wanawaza kwenye vichwa vyao kama aliyekuwa kocha wa Chelsea Jose Mourinho anaweza kutua old Trafford na kuwanoa mashetani wa jiji la Manchester.

Wakati huu ambao Pep Gurdiola anatarajiwa kuwanoa wapinzani wa miamba hiyo pale Etihad bila shaka hamu ya mashabiki wa Man united ni kuona anatua kocha bora ambaye anaweza kukabiliana na changamoto za ushindani kwa wapinzani hao na timu zingine ambazo zina matarajio ya kujipanga zaidi kama Liverpool na Chelsea.

Jose Mourinho maarufu kama "the special one" amekuwa na soka lisilotabirika na mara nyingi ameweza kufanya vizuri katika timu kadhaa alizokuwa nazo ikiwemo Porto, Chelsea, Intermilan na Real Madrid, hivyo wakati huu ambao mreno huyo anakitolea macho kibarua cha Old Trafford ni wakati huu hamu ya mashabiki wa timu hiyo ipo kwake kutokana na kufanya vibaya kwa kocha Louis van Gaal.

Katika misimu 7 ambayo Barcelona amesambaza wimbi la ubabe kwa mahasimu wao Real Madrid ni Mourinho pekee ambaye aliweza kutunishiana misuli na kocha Pep Gurdiola na kubeba kombe la liga mara 1 katika kipindi cha miaka miwili alipokuwa na wababe hao wa Santiago Bernabeu.

Ingawa Mourinho hana soka lenye kuvutia uwanjani lakini amekuwa mwenye kutimiza malengo yake kwa kile anachopanga katika timu husika na hili ndilo jambo pekee ambalo Raisi wa Intermilan Massimo Morati hatasahau katika maisha yake hii inamfanaya kumwitaji Jose Mourinho ambaye aliinua ndoto za intermilan akiwa na timu hiyo.

Binafsi Mourinho ni kocha mwenye mbinu nyingi kulingana na mpinzani anayekutana naye na aina ya mpira wauchezao. Licha ya kuwa chini ya LvG wakati alipokuwa masidizi wake pale Barcelona lakini Mourinho aliweza kumshinda kocha huyo katika mchezo wa fainali wa kombe la mabingwa barani ulaya (UEFA) kwa kumpa kichapo cha mabao 2-0 hii inaonesha Mourinho ni mbunifu zaidi kuliko LvG.

Bila shaka Sir Alex Ferguson anafahamu shughuli ya mwanaume huyo ambaye hakuwahi kumfunga kipindi chote alichokuwepo kwenye ligi ya EPL, nadhani ni Mourinho pekee anaweza kuvaa viatu vya kocha huyu na kurejesha heshima ya mashetani hao katika ligi ya EPL.

Binafsi Ferguson hakuwa na soka la kumiliki mpira muda mwingi kama Hispania, au lile soka alilopeleka kocha LvG kwa timu hiyo. Ferguson alitumia zaidi wachezaji wenye nidhamu na wanaopenda kujituma uwanjani na kwa staili yake ya soka aliweza kuvunja ufalme wa liverpoo katika kipindi cha miaka 26 alichokuwepo pale Old Trafford.

Katika kipindi cha miaka cha miaka ishirini ya Ferguson hakukuwa na lile soka la LvG lakini heshima ilikuwepo pale Old Trafford, ni wakati huu namuona Mourinho ndiye kocha pekee ambaye anaweza akaimudu united na Pep Gurdiola.

Kama Ferguson alimuuza Christian Ronaldo na kumnunua Antonio Valencia kutoka Wigan Athletics bila shaka LvG asingweza kufanya hivyo angefikiria nyota zaidi. Tukumbuke Ferguson alibeba taji la EPL na kuuvunja rasmi utawala wa Liverpool.

Kama Wesley Sneidjer, Walter Samuel, Lucio na Diego ni wachezaji waliokuwa wamepoteza umaarufu katika timu zao licha ya kufanya vizuri lakini Jose Mourinho pekee aliyeifanya Intermilan kuwa bora ikibeba taji la Serie A mara 2 na lile la klabu bingwa Ulaya na kujitengenezea heshima na historia katika timu hiyo.

Watu wanajiuliza kama Mourinho ataweza kudumu muda mrefu katika timu hiyo ya Old Trafford bila shaka Mourinho atadumu zaidi kwa sababu ana ndoto za muda mrefu za kuwafundisha mabingwa hao na kuweka historia katika timu hiyo. Ni Mourinho pekee ambaye anafanana na Ferguson katika misimamo, kujenga nidhamu, kutumia wachezaji wanaojituma kuliko nyota wenye majina yao duniani na kuhamasisha.

Nadhani Man united itamtumia kocha Mourinho kurejesha heshima yao pale Old Trafford, ni matumaini yangu kuwa Mourinho ndiye kocha pekee ambaye atatua Manchester united na kuvaa viatu vya Sir Alex Ferguson ipasavyo kwa asilimia 80.

Comments