Huenda siku ya jana ilikuwa ya matarajio ya wengi pengine Ubelgiji ingefuzu kwenye hatua ya nusu fainali dhidi ya Wales lakini badala yake mambo yakawa kinyume na matarajio ya wengi.
Kwa wana mpira si jambo la kushangaza sana, licha ya Ubelgiji kuwa na kizazi cha dhahabu karne hii lakini wanashindwa kufanya vizuri mashindanoni, pamoja na kuwa kwenye nafasi nzuri kwenye viwango vya FIFA duniani lakini Ubelgiji imeshindwa kutetea hadhi yake.
Hapa ndipo unapoona tofauti ya Ubelgiji na timu kama Italy, mara nyingi mashindano ya muda mfupi sana hayahitaji ufundi mwingi yanahitaji zaidi mbinu, na jinsi kupata matokeo kwa kuwa ni mechi saba pekee bingwa huwa nazo kuna nafasi ndogo ya kuonesha ulichinacho ila kuna nafasi kubwa ya kutengeneza matokeo.
Hilo sasa linaigharimu Ubelgiji, mwalimu Marc Wilmot ameshindwa kuwatengeneza wachezaji wake kimashindano, Wengi wapo kwa ajili ya kuonesha walichonacho na hapo ndipo kwenye tatizo hili ni jambo baya kidogo pamoja na yote Ubelgiji imekosa maelewano katika eneo la ulinzi na fowardi yao.
Nikianacho kwa Eden Hazard ni juhudi binafsi licha ya kuwa ameweza kuwa nyota kwenye timu hiyo, Hakuna mchanganyiko wa mahesabu ulioundwa na mwalimu Marc Wilmot kwa ajili ya Eden Hazard, Kevin De Bruyne au Yannic Carrasco na Romelu Lukaku.
Najisikia raha nikimwona Emmanuelle Giaccherin akifanya mambo makubwa na Italy, amekuwa muhimili wa Antonio Conte usishangae akitua chelsea wakati wowote licha ya kukosa namba ya kudumu Sunderland ambayo ilimtoa kwa mkopo, lakini angalia anachokifanya na Italy ni kupambana na kutekeleza majukumu ana hali ya kujitoa kwenye timu.
Wachezaji wengi wa Italy wapo kimashindano na wanaandaliwa kwenye hali hiyo, hata kama wengi wao hukosa nafasi kwenye timu zao lakini ni wepesi wa kutekeleza majukumu katika taifa lao. Walichokifanya Wales hakitofautiani sana na Italy walicheza kwa hali, mbinu na kujitoa.
Ukiangalia kasi ya Wales ilikuwa na utofauti mkubwa na ile ya Ubelgiji, Wales walifika kwa madhara licha ya kuondoka wachache kwa mashambulizi ya kushtukiza lakini yalizaa matunda, na ndio waliibuka kifua mbele kwa magoli 3-1, sawa ule ushindi walioupata walipokutana kwenye makundi ya kufuzu fainali hizi.
Leo hii PSV anaonekana mfalme kuliko Ajax katika kipindi cha misimu minne, tofauti ni kuwa Ajax chini ya Frank De Boer wanacheza soka la shule hawawezi soka la kazi linalopigwa na PSV, na hilo ndio sababu pekee iliwafanya PSV kuwapokonya tonge mdomoni katika mechi ya mwisho ya kugombania ubingwa baada ya Ajax kupata sare.
Kitendo cha PSV kukomaa na Atletico Madrid hadi hatua ya penati katika michuano ya klabu bingwa barani Ulaya ni wazi PSV ilikuwa kimashindano licha ya kwamba hawana soka la kuvutia uwanjani lakini wana soka la kupata matokeo na ndiyo maana ilikuwa rahisi kwao kuvuka mbele ya Manchester united.
Nadhani Marc Wilmot akajipange upya baada ya kuchemsha kwenye michuano hii, akafikirie kutengeneza Ubelgiji yenye ushindani ili mashabiki wake wakafurahie kule Russia panapo majaliwa katika michuano ya kombe la dunia mwaka 2018, akajifunze namna Italy ilivyofanya na jinsi gani Wales walimng'oa kwenye mashindano nadhani atakuwa na timu bora zaidi.
Comments
Post a Comment