SHIRIKISHO la Soka Tanzania (TFF) hatimaye limetoa ratiba ya Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) Bara msimu wa 2016/17.
Kwa mujibu wa ratiba hiyo iliyotolewa na Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, ligi hiyo itaanza rasmi kutimua vumbi, Agosti 20 ambako Simba itaanza kwa kuumana na Ndanda ya Mtwara, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Siku hiyo hiyo, Azam itaonyesha ubabe na African Lyon, mechi itakayopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex.
Katika ratiba hiyo, mahasimu wa soka nchini, Yanga na Simba wataonyeshana ubabe Oktoba Mosi mwaka huu katika mechi ambayo Yanga watakuwa wenyeji.
Wiki mbili baada ya mechi hiyo, Yanga ambao ndio mabingwa watetezi watakuwa na kibarua kingine kigumu dhidi ya Azam, timu iliyoshika nafasi ya pili.
Kagera Sugar wataanza na Mbeya City Uwanja wa Kaitaba, Bukoba, Toto Africans na Mwadui FC Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza, Stand United na Mbao FC Uwanja wa Kambarage, Shinyanga, Mtibwa Sugar na Ruvu Shooting Uwanja wa Manungu, Turiani, Morogoro na Majimaji na Prisons Uwanja wa Majimaji Songea.
Mabingwa watetezi, Yanga SC wataanza kutetea taji lao Agosti 31 dhidi ya JKT Ruvu Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Na hiyo ni kwa sababu TFF imewapa nafasi ya kujiandaa na mchezo wao wa Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya TP Mazembe utakaochgezwa Agosti 23 mjini Lubumbashi, DRC.

Comments
Post a Comment