Chelsea, Man united walivyoacha mbachao kwa msala upitao

Pogba (kushoto), Lukaku (kulia) wakicheza mpira wa kikapu 

Kama ni kweli mvumilivu hula mbivu basi wahenga walikuwa sahihi katika usemi huu, wakati fulani tunatakiwa kuvumilia katika baadhi ya mambo ikiwemo na malezi ya vijana pia. Leo kuna vijana wawili wamekuwa wamekuwa nyota duniani licha ya Manchester united na Chelsea kushindwa kuona umuhimu wao.

Kuna tukio moja lilifanyika Las Vegas wiki mbili zilizopita ambapo Kiungo Paul Pogba akiwa na mshambuliaji wa Chelsea Romelu Lukaku walionekana kwa pamoja wakicheza mpira wa kikapu kwa raha zao wakiwa mapumzikoni baada ya majukumu mazito ya kutumikia timu zao za taifa.

Wakati nyota hao wakiendelea kuponda raha na timu zao za zamani zilikuwa zikiumiza kichwa ni namna gani wanaweza kuwarejesha wachezaji hao ambao kwa sasa wana thamani kubwa kuliko ilivyokuwa hapo awali.

Romelu Lukaku alionekana mwenye kipaji cha hali ya juu katika kufumania nyavu na ndipo akaletwa Chelsea kama mrithi wa Didier Drogba akitokea Anderlecht ya Ubelgiji mwaka 2011 Chelsea ilidumu nae kwa misimu mitatu licha ya kumtoa kwa mkopo katika timu ya Westbrom na baadae Everton ambako alikuwa nyota.

Licha ya kutua kwa mkopo Everton 2013/14 bado Lukaku akidhihirisha kuwa yeye ni bora na baadae Everton ilimnunua moja kwa moja nyota huyo kwa ada ya uhamisho wa paundi milioni 28, kuanzia mwaka 2014 hadi sasa

Matokeo ya kukosa uvumilivu yanaigharimu timu ya Chelsea kumrudisha mchezaji huyo kwa kwa dau la paundi milioni 60 ni mara mbili ya ile pesa waliyotumia mwanzo Everton kumtoa nyota huypo katika klabu ya Chelsea.

Hivi karibuni iliwahi kutokea pia kwa Nemanja Matic ambaye aliuzwa kwa bei kuelekea Benifica lakini pia aliigharimu Chelsea kutumia dau la paundi milioni 24 kumrejesha kiungo huyo darajani kwa mara nyingine.

Kwa upande wa Manchester united picha ya Chelsea inajirudia kwao kwa mara nyingine ni kutokana na Paul Pogba kuwika kwenye ulimwengu wa soka akiwa na Juventus, licha ya Pogba kutua Juvetus akiwa na miaka 18 aliweza kuimarika chini ya Conte na kuwa nyota kwenye dunia ya soka.

Ingawa Paul Scholes alisema wazi kuwa Pobga hafikii thamani ya paundi milioni 100 kusajiliwa Manchester united lakini amesahau soka la sasa limeegemea kwenye misingi ya  biashara, mafanikio ya haraka na kutengeza mshiko wa kutosha.

Ndicho kinachokea kwa Pogba leo ametamba akiwa na Juventus na nyota yake inang'aa kuliko baadhi ya nyota wenye majina makubwa kama Luka Modrick na James Rodriquez licha ya kuwa na vipaji vya hali ya juu kuliko mfaransa huyo.

Ndiyo soka la sasa lilivyo haliitaji miaka mingi kutengeneza biashara bali linataka uvumilivu kumtunza mchezaji anayeonesha kipaji kwenye soka. hakuna jambo la kushangaza kwa N'golo Kante  amepigwa bei ya paundi milioni 30 kutua Chelsea au Mahrez mahrez kuuzwa kwa gharama hiyo licha ya kuwa hakufikisha hata kiasi cha paundi milioni 1 akitokea Le Havre inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini  Ufaransa.

Leo kante amepigwa bei mara 5 ya pesa aliyonunuliwa, hakuna shaka biashara imetawala soka la sasa, licha ya kuwa na msimu mmoja wa mafanikio na Leicester city lakini Leicester imevuna faida mara dufu kwa mchezaji.

Ndivyo ilivyo kwa Everton na Juventus ambao wameacha vinywa vyao wazi wakisubiri kutafuna mabilioni ya Manchester na Chelsea ambao walikosa uvumilivu na kutanguliza biashara mbele. Wakati Pogba anasubiriwa kama mfalme pale Old Trafford ambako miaka minne iliyopita alikuwa si lolote si chochote akitokea Le Havre ya Ufaransa.

Ni wakati ndipo Chelsea kwa upande wao  wanapoumiza kichwa kutoa mara mbili ya pesa waliypokea mwanzo huenda Everton ikapiga mpunga zaidi kuliko wao, bila shaka haya matokeo ya kukosa uvumilivu katika kuongoza vipaji vya wachezaji.

Wachezaji hawa ambao wote wana miaka 23, leo hii wanaiumiza dunia lakini wenyewe wanakula bata huko Marekani kwa kuwa wapo watu wanaoshughulikia biashara yao. Kweli Man united na Chelsea walicha mbachao kwa msala upitao.

Comments