Conte ameivika roho ya ujasiri Chelsea


Inawezeka kilichosemwa na Eden Hazard kuhusiana na Chelsea kubadilika chini ya kocha wa sasa Antonio Conte ni kweli baada ya Chelsea kusakata kabumbu kubwa dhidi ya West Ham jana.

Hazard aliahidi kufanya mambo makubwa chini ya Conte na kuweka ahadi ya kurejesha kiwango chake kwenye ubora kama ilivyokuwa hapo awali, bila shaka Hazard alicheza katika kiwango cha juu sana.

Chelsea imebeba roho ya ujasiri sasa katika mapambano mapya ya EPL 2016/17, jana wakiwa kwenye uwanja wa nyumbani kwa pamoja wamecheza kwenye kiwango cha juu.

Kuna mabadiliko makubwa kwa Branslav Ivanovic, Nemanja Matic na Oscar ambao hawakuwa kwenye kiwango kizuri msimu ulipita lakini sasa wamerejea kwenye kiwango chao vile tunavyofahamu walivyokuwa.

Kwa upande wa N'golo Kante alicheza vizuri na kuongoza vema safu ya kiungo hali iliyofanya Matic na Oscar kucheza katika kiwango cha juu.

Pia Diego Costa anaonekana kurejea vizuri, jana alicheza kwa juhudi kubwa na kupelekea Chelsea kuibuka na ushindi baada kuifungia timu yake bao la pili na kuyafanya matokeo kuwa 2-1 wakiendeleza rekodi yao dhidi ya West Ham pale Stamford Bridge.

Conte binafsi amesifu juhudi za Strika huyo, kutokana na kiwango bora alichoonesha. Alipoulizwa kuhusu Costa alijibu, " nadhani Costa ameonesha anachotakiwa kufanya, alijituma na kutafuta bao la ushindi kwa juhudi kubwa, kiwango chake ni bora."

Hata hivyo Conte amesifu timu yake kiujumla bila kumsahau Mbrazil Willian ambaye yeye amefungua ligi na moto wake ule ule aliomaliza, alikuwa na moja waliokuwa tishio katika kuisambaratisha ngome ya West Ham united.

Nadhani Conte amefanikisha jambo la kwanza muhimu, ameinua hali ya wachezaji wa Chelsea na sasa anajiandaa kuwakaribisha mashabiki wa Chelsea kwenye Himaya yake.

Comments