Yanga kazini leo, Lyon nayo yataka pointi 3


Timu ya Yanga leo inaanza harakati zake za kutetea ubingwa wa ligi kuu ambapo itashuka dimbani katika mtangange wa ligi hiyo dhidi ya African Lyon kwenye uwanja wa Taifa.

Yanga imeondoka rasmi kwenye michuano ya kombe la shirikisho na sasa mawazo na nguvu zao zimehamia rasmi ligi kuu kabla ya kuanza tena kwa michuano ya klabu bingwa Afrika.

Kocha wa Yanga Hans van Der Pluijm amesema kuwa timu yake itashuka dimbani kusaka pointi, na lazima iondoke na pointi 3.

"Pamoja na kuwa hatukuwa na muda wa kutosha lakini ushindi ndiyo malengo dhidi Lyon." Alisema Pluijm

"Tumeondoka kwenye michuano ya kombe la shirikisho, watu hawapaswi kujenga dharau juu yetu bado tuna timu bora." Aliongeza Pluijm.

Kwa upande wa kocha sasa wa African Lyon ambaye ni raia wa Ureno Bernardo Teveras amesema kuwa hana hofu na Yanga kwani amewaona mara nyingi kwenye mechi mbali mbali za kimataifa.

"Kupata pointi 3 kwa Yanga inawezekana bila shaka timu yao inafungika, nimeiona mara nyingi kwenye mechi za kimataifa siyo timu ngeni machoni mwangu." Alisema Teveras.

Comments