Timu ya Maji maji ndiyo timu pekee iliyoruhusu mabao mengi zaidi tangu kuanza kwa ligi kuu ya Vodacom 2016/17 hadi sasa wamecheza mechi nne na kuruhusu bao 9 kuingia kwenye nyavu zao.
Maji maji ilipoteza mechi ya kwanza dhidi ya Prisons ikiwa nyumbani ilifungwa bao 1-0, ikafungwa 2-1 na Mtibwa, ilisafiri kwenda Chamanzi ambapo walifungwa bao 3-0 na Azam na mechi ya mwisho ilifungwa bao 3-0 na Yanga.
Matokeo hayo yanadhihirisha wazi kuwa safu ya ulinzi ya Majimaji ni dhaifu sana kulinganisha na timu zingine za ligi kuu. Hakuna ubishi ni lazima timu hiyo ichukue tahadhari kabla ya hatari.
Kufungwa goli 9 katika mechi nne ni jambo hatarishi kwenye timu, nadhani Majimaji wanatakiwa kuwa namba moja kuhakikisha wanasajili wachezaji wa kuongeza nguvu kwenye safu ya ulinzi lakini mbali na usajili wa beki Majimaji inatakiwa kunoa safu yake ya ushambuliaji.
Idadi ya goli moja ambayo Majimaji imefunga ndani ya mechi nne inaonesha ni jinsi gani timu hiyo imekosa watu makini wa kufumania nyavu. Mbali na mapungufu ya ulinzi kuna silaha nyingine ya kujilinda, nayo ni kufunga magoli na hiyo ndiyo njia pekee ya kumtia hofu mpinzani wako.
Mbaya zaidi Majimaji wanaonekana kuwa na kiungo imara na kukosa nguvu eneo la ulinzi, eneo la strika, hii haina maana kwenye timu ni sawa na kazi bure. Napenda Majimaji ijifunze kupitia Aston Villa, binafsi niliipenda Villa ilikuwa na mpira mzuri katikati lakini ilikosa nguvu nyuma na mbele na ndiyo maana leo hii inapambana kupanda daraja.
Villa ilidhoofika mbele na nyuma na ndiyo maana ilishuka daraja ikiwa ni moja ya timu yenye pointi chache ikiwa imefungwa magoli mengi zaidi kulingo timu ambazo ilishuka nazo daraja. Nataka Majimaji ijipange upya na ijifunze kupitia Villa vinginevyo ni wazi watashuka daraja huku wakiutamani utamu wa ligi kuu.

Comments
Post a Comment