Ni Kweli Lufunga anastahili kumuweka Murshid benchi?


Bila shaka naisifu Simba kwa usajili wa beki wa zamani wa Mamelodi Sundown ya South Africa mzimbabwe Method Mwanjali ambaye kwa sasa anaonekana kuiongoza vema safu ya ulinzi, anaonekana kuwa imara na mtulivu tangu alipoanza kuitumikia Simba.

Kocha wa Simba Joseph Omog anaonekana kuvutiwa na mpango wa kuwatumia Method Mwanjali pamoja na Mtanzania Novaty Lufunga, ingawa Simba imeanza vizuri lakini naona mapungufu na makosa ya wazi kwenye safu ya ulinzi ya Simba.

Mwanjali ni mtulivu na mwenye kasi ya kawaida uwanjani hali kadhalika iko hivyo kwa upande wa Novaty Lufunga ambaye hatofautiani sana aina ya utulivu wake na Mwanjali. Hili litaigharimu Simba siku kutokana na kuweka watu wa aina moja kwenye safu ya ulinzi.

Binafsi nafikiria mwalimu Joseph Omog angeliangalia upya suala la kumuweka benchi beki wa Uganda Juuko Murshid. Nadhani Murshid ni tofauti kidogo na Novaty Lufunga, anatumia nguvu, yuko haraka na beki mwenye maamuzi Sahihi nadhani anaweza kutumika vema na Method Mwanjali.

Naitazama Simba kwa makini, katika mechi nne ilizocheza imeshindwa imeonesha udhaifu mkubwa katika kucheza mipira ya juu, hii ni hatari, kwa upande wangu Novaty ni mvivu kidogo namaanisha ana hali ya upambanaji kama ilivyo kwa Juuko Murshid.

Simba ambao wana ndoto za kuipiku Azam na Yanga msimu huu nadhani ukuta wao una kibarua kigumu cha kuwazuia Donald Ngoma, Amis Tambwe au John Boko wa Azam wasipeleke maumivu kwenye lango lao, endapo timu ya Simba itapambana na Washambuliaji au mabeki wa kati ambao wana umakini mkubwa na mipira ya vichwa ni rahisi kufungwa.

Nikiziangalia Simba, Azam na Yanga naiona Simba ina ukuta dhaifu kuliko hizo timu mbili, bado mwalimu Joseph Omog ana nafasi ya kubadilisha maamuzi. Novaty Lufunga ni mchezaji mzuri lakini hajafikia vigezo vya kumuweka benchi Juuko Murshid nje lakini mbaya zaidi Lufunga hawezi kupambana zaidi ya vile anavofanya Juuko Murshid.

Kwa upande wa kufuta makosa yasiyo na lazima, kufanya tackling nyingi na kucheza mipira juu nadhani Juuko Murshid atakuwa na msaada mkubwa kwa Method Mwanjali kuliko Lufunga. Nakumbuka jinsi Lufunga alivyopata shida kwa John Boko kwenye mechi ya mwisho waliyokutana Simba na Azam, nakumbuka Ngoma alivyomchomoa beki huyu Simba kwa kadi nyekundu.

Je Kuna mabadiliko kwa Lufunga? Nadhani bado Juuko anastahili kuwepo kwenye kikosi cha kwanza cha Simba. Simba inakutana na Azam kwenye mechi inayokuja nadhani hii ndiyo changamoto kubwa ya kwanza kwa timu hii ambayo bado haijacheza hata mechi moja nje ya mkoa wa Dar es Salaam kule ambako kunaitaji umakini wa hali ya juu kupambana na kucheza mipira ya juu.

Si mbaya leo ukisikia Kelvin Yondani anasugua benchi kwa ajili ya Adrew Vicent 'Dante', anayeweza kwa wakati huo anastahili zaidi kumweka nje mchezaji mzembe, Leo hii Eric Bailly anamshawishi Mourinho na ndiyo maana Phil Jones anasugua benchi kwa ajili ya jembe hilo kutokea pande za Ivory Coast,

Nawaachia wapenzi na wadau mbalimbali wa soka na mashabiki wa Simba watafakari juu ya jambo hili, Vinginevyo kuizuia Safu ya Ushambulaji  Yanga, Azam na timu za mikoani kama Prisons kuna kazi kubwa mbele ya Simba kwa ukuta huu wa Joseph wa Omog.

Comments