Ranieri kama ananyata huku anataka


Baada ya kusaka historia yake binafsi ikiwa ni mara kwanza kutwaa ubingwa wa ligi kuu tangu alipoanza kuwa mwalimu wa soka, Claudio Ranieri alifanya hivyo akiwa na Leicester. Ingawa wingi wa wapenzi wa soka wanaamini ilikuwa kama zari Leicester kutwaa ubingwa wa EPL lakini ipo haja ya kuwapongeza mabingwa hao ambao walijitoa sana kupigania ubingwa.

Ikumbukwe kuwa msimu uliopita Ranieri hakuweka wazi nia yake ya kushindania ubingwa ingawa licha ya uelekeo mzuri kwenye timu yake, alisisitiza malengo yake ni kuwepo kwenye nne bora ya EPL, lakini hatimaye alitangaza nia ya ubingwa zikiwa zimebaki siku chache kabla ya kumalizika kwa ligi kuu.

Jana kabla ya kufungwa kwa dirisha la usajili Ranieri alikuwa amekamilisha usajili wa mshambuliaji wa Sporting Lisbon ya Ureno Sliman Islam, ikiwa ni wiki chache tangu afanye usajili wa Mussa. Ranieri ameanza kujiami pia ameanza kuweka tahadhari kabla ya hatari.

Kocha huyo anafahamu vema kuwa ana kibarua kizito katika ligi ya mabingwa Ulaya na EPL, na hivyo anaongeza nguvu kwenye kikosi chake, ingawa ni siku chache tangu ligi imeanza hii hainipi sababu ya kumtoa Leicester kwenye nne bora au kwenye mbio za ubingwa, ingawa N'golo Kante amepunguza kitu kikubwa kwenye sehemu ya kiungo nadhani mambo yanakwenda kuwa sawa kwenye timu hiyo wakati wowote.

Ingawa Ranieri anajua wazi kuwa Chelsea, Manchester city, Manchester united united zinarudi vizuri zikiwa na hali ya ushindani katika ligi naamini hali hii haimvuji moyo Ranieri nadhani anazidi kujiimarisha na kuiongoza timu yake izidi kujituma

Kwa upande wangu Ranieri ana mtazamo wa mbali kuliko watu wanavohisi, kwa Ranieri ana malengi ya ubingwa nyumbani hata katika kombe klabu bingwa barani Ulaya. Anataka kufanya maajabu siyo yale yaliyotokea EPL bali hata kwenye ligi hiyo.

Wengi wanadhani Ranieri ana mipango kwenye ligi ya mabingwa pekee hii si kweli, kocha huyo ana ndoto za mbali na ndiyo maana kwa sasa ana washambuliaji watano akiwemo Jamie Vardy, Mussa, Slimani, Ulloa pamoja na shinji Okazaki. Ranieri ameshanoa kisu, shoka, panga hata jembe vina makali pia ametegesha silaha zake zote kwa sasa ana kikosi kipana zaidi.

Ranieri kwa sasa amepunguza presha ingawa sisi hatuoni hilo lakini ukweli ni kuwa endapo Jamie Vardy ataingia kwenye majeraha au matatizo mengine tofauti atakuwa na washambuliaji mbadala wa kuendana na mfumo wake katika mashindano yote ikiwemo EPL na klabu bingwa Ulaya.

Hakuna mtu asiyependa mafanikio binafsi maishani, na kujenga historia endapo kocha huyo ataweza kutetea ubingwa au kuziweka chini timu za Manchester city na Man united licha ya usajili mkubwa waliofanya bado Ranieri ataendelea kuwa shujaa.

Kwenye mechi kati ya Leicester city na Arsenal niliona hali ya upambanaji kwenye timu ya Leicester, ingawa bado tunaifikiria Leicester kuwa ni timu ndogo, Manchester city pia ilianza hivyo na taratibu ilianza kuangamiza kabisa ufalme wa Liverpool kwenye nne bora ya ligi kuu.

Ukweli ni kuwa Ranieri hawezi kuweka nia yake ya mafanikio wazi kama ilivyo kwa Jose Mourinho ambaye huongea na kutenda bali yeye anataka kufanya kimya kimya nina uhakika kuna sehemu ya mafanikio ambayo kocha huyo anataka kuyafikia.

Binafsi sioni kama Ranieri anataka kuwa nje ya nne bora au chini ya Liverpool, Man utd, Man city au Chelsea pamoja na Arsenal, na ndiyo maana nikasema Ranieri ni mtu anayenyata huku anataka, anafanana na mfano wa mnyama fisi mwenye aibu lakini anatamani.

Comments