Stars yakamilisha ratiba kwa Kichapo


Taifa Stars imekamilisha mechi zake za kuwania kufuzu kucheza kombe la mataifa afrika (AFCON) kwa kichapo cha bao 1-0 dhidi ya Nigeria.

Goli pekee la mechi hiyo limepatikana katika dakika ya 76 la mshambuliaji wa Manchester City Kelechi Iheanacho limeendeleza rekodi ya Stars kushindwa kupata ushindi mbele ya Nigeria ambapo kwa mujibu wa rekodi, Stars haijafanikiwa kupata ushindi mbele ya Super Eagles tangu timu hizo zilipoanza kukutana.

Stars ilisafiri hadi Nigeria kwenda kucheza mchezo wa kukamilisha ratiba katika Kundi G ikiwa ni mechi ya kutafuta nafasi ya kufuzu kucheza fainali za michuano ya mataifa ya Afrika (AFCON 2017) nchini Gabon.

Timu ya Nigeria ndiyo walioshambulia sana na washambuliaji wake Victor Moses na Alex Iwobi walipoteza nafasi nyingi zaidi za kufunga.

Stars ingepigwa mabao mengi lakini mlinda lango, Aishi Manula alikuwa imara kuokoa michomo mingi ya hatari.

Hadi hatua ya makundi inamalizika, Stars haijafanikiwa kupata ushindi katika Kundi G baada ya Chad kujitoa kwenye kundi hilo kutokana na matatizo ya kifedha.

Ushindi pekee wa Tanzania ulikuwa ni dhidi ya Chad ambapo Stars ilipata ushindi wa goli 1-0 ugenini lakini ushindi huo ulifutwa baada ya Chad kujiengua.

Comments