Bado Kipre Tchetche anaitafuna Azam FC.


Licha ya timu ya Azam kufanya usajili wa nyota kadhaa akiwemo Bruce Kangwa pamoja na Ya Thomas bado hawajapa mtu sahihi ambaye amerithi majukumu na ubora wa Kipre Tchetche alitimka Azam kabla ya kuanza kwa ligi.

Mapema kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa ligi kuu Kipre Tchetche aliomba kuondoka kwenye timu hiyo, ingawa Azam waliweka ngumu katika siku za mwanzo lakini ilibidi wamwache Kipre Tchetche ambaye ameonekana kuchoshwa na maisha ya Tanzania.

Azam wanakosa wachezaji maalum wa kuamua matokeo kwenye mechi zao, mpaka sasa Azam haijapata ushindi kwenye mechi tano tano ilizocheza ikiwa na sare pamoja na kufungwa mechi moja na Stand United mkoani Shinyanga.

Kasi na maarifa ya mshambuliaji Kipre Tchetche ilikuwa na nguvu kubwa katika safu ya ushambuliaji wa Azam. Ingawa Ya Thomas pamoja na Bruce Kangwa ambao kwa sasa wanaungana na John Bocco kwenye safu ya ushambuliaji wana kasi kubwa uwanjani lakini wamekosa maarifa pia wamekosa ubunifu ukilinganisha ilivyokuwa kwa Kipre Tchetche.

Ya Thomas si mchezaji anayefanana na Kipre Tchetche ingawa ana kasi kubwa uwanjani lakini amekosa ubunifu wa kuitikisa  ngome pinzani hali kadhalika iko hivyo kwa Bruce Kangwa ambaye licha ya uwezo wake mkubwa kwenye kushambulia na kukaba bado ameshindwa kuwa msaada zinapohitajika juhudi binafsi za mchezaji kuokoa jahazi isizame.

Jana wakati Azam ilipokuwa inachuana kwenye uwanja wa Taifa na Yanga ni rahisi kugundua mapungufu ya Azam kwenye safu yao ya ushambuliaji. Kipindi cha pili Azam walianza kushambulia lango la Yanga wa kasi zaidi Ingawa Ya Thomas na Bruce Kangwa walipata nafasi mbili za wazi lakini walishindwa kuiandikia Azam bao.

Kwenye mechi ya jana Azam ilitengeneza nafasi nyingi zaidi ambazo zilikuwa hatarishi kuliko walivyofanya Yanga. Ubunifu unaigharimu Azam, ingawa wancheza mpira mwingi uwanjani lakini wanashindwa kutumia nafasi wanazopata.

Si ajabu pale Azam ilipofungwa na Stand ingawa ilitawala mpira zaidi kuliko Stand united, makosa yaliyowanyima pointi jana ndiyo hayo yaliyowagharimu na kupoteza pointi kwa Stand united. Azam ilipata nafasi ambazo hazipungui sita walicheza na Stand united lakini walishindwa kuzitumia ipasavyo.

Kama unaifahamu Azam ilivyokuwa miaka miwili nyuma basi bila shaka hakuna ubishi kuwa Kipre Tchetche ni pengo Azam FC, na baadhi ya wachezaji akiwemo John Bocco wanaendelea kukumbuka shughuli ya mshambuliaji huyo alipokuwa uwanjani na timu hiyo.


Comments