Kagera yawafungia Casillas, Kyarazi kwa tuhuma za kupokea Hongo.


Uongozi wa timu ya Kagera Sugar umewafungia wachezaji wawili wa timu hiyo gollikipa Hussein Sharrif 'Casillas' na Eric Kyarazi kwa tuhuma za  kuihujumu timu ilipofungwa bao 6-2 na Yanga.

Taarifa hizo zimethibitishwa rasmi na katibu mkuu wa timu hiyo Hamis Madaki kuwa wachezaji hao wamesimamishwa kwa muda usiojulikana ili kupisha uchunguzi wa tuhuma hizo.

"Tunaendelea na uchunguzi kutokana  na kuonekana kwa hujuma kwenye mechi yetu na Yanga, ili kupisha uchunguzi wa kina tumeona nyota hao wakae kando kwanza.

"Aina ya Magoli tuliyofungwa kila mtu aliyaona yanatia sana wasiwasi, suala si kufungwa magoli mengi tatizo ni aina ya magoli tuliyofungwa na Yanga.

"Tumeshawakabidhi barua zao, nadhani barua zimeonesha kila kitu kuwa tumewasimamisha kwa muda usiojulikana."Alisema Madaki

Katika mchezo huo Hussein Sharif alifungwa magoli matatu kipindi cha kwanza na kufanyiwa mabadiliko kipindi cha pili kumpisha David Burhan ambaye pia alifungwa magoli matatu .

Pia beki Eric Kyaruzi amefungiwa kutokana na kurudisha pasi fupi kwa kipa wake ambapo Donald Ngoma aliuwahi mpira huo na kufunga bao.

Comments