Mshambuliaji wa Simba Shiza kichuya ameibuka shujaa katika uwanja wa taifa baada ya kuchomoa dhidi ya Yanga na kuyafanya matokeo kuwa 1-1.
Kipindi cha kwanza Yanga ilipata bao la kuongoza kupitia Amis Tambwe aliyefunga dakika ya 27 ya mchezo huo ingawa goli hilo lilileta utata kutokana na Tambwe kuusapoti mpira kwa mkono wakati akigeuka.
Kwa muda usiopungua dakika tano mechi hiyo iliweza kusimama kutokana na vurugu za mashabiki wa simba ambao baadhi yao waliweza kung'oa sehemu ya viti kutokana na bao pamoja na kutolewa nje kwa kadi kwa nahodha Simba Jonas Mkude.
Hata hivyo Simba ilionekana kurudi kwa utulivu kipindi cha pili na kuweza kuutawala mpira muda mwingi licha ya kuwa pungufu kwa mchezaji mmoja na kuweza kupata bao la kuchomoa kupitia Shiza Kichuya aliyefunga kwa mpira wa kona ambao ulizama wavuni moja kwa moja.
Matokeo hayo bado yanaifanya Simba kutembea sambamba na rekodi ya Stand united ambayo haijapoteza mechi hadi sasa na kuendelea kutamba juu ya msimamo wa ligi hiyo.

Comments
Post a Comment