Maskini Patrick Liewig anatuachia Stand united ikiwa kwenye ubora


Zipo taarifa kuwa kocha wa Stand united Patrick Liewig yuko jijini Dar es Salaam akifanya taraibu za kutimka Bongo kuelekea kwao.

Jioni ya Leo Stand united itachuana na African Lyon katika uwanja wa Kambarage na kocha Patrick Liewig hatakuwepo katika mtanange huo.

Tangu uongozi wa Stand united ulipoingia kwenye mgogoro, kampuni ya uchimbaji wa madini ACACIA ambayo ndiyo ilikuwa ikidhamini timu hiyo iliamua kujitoa na sasa hali ya kifedha si nzuri sana kama ilivyokuwa hapo awali.

Ni juhudi kubwa zimefanywa na kocha huyo ambaye ameiongoza Stand united kwenye mechi 9 akiwa hajapoteza mchezo wowote hadi sasa ikiwa ni pamoja na kuifunga timu ya Yanga pamoja na Azam.

Tamaa za watu wachache zimeiponza Stand united, leo hii Liewig anaondoka kwa sababu timu hiyo imeshindwa kumlipa mshahara kocha huyo na sasa italazimika kutafuta kocha mzawa na huenda Stand isiwe ile tuliyoizoea chini ya Liewig.

Kocha huyo anaondoka akiwa anaiacha timu hiyo ikiwa kwenye ubora, Liewig amekuwa akifanya vizuri tangu alipotua Stand united timu hiyo imeweza kusimama vema kwenye msimamo wa ligi kuu hadi sasa ikiachwa pointi moja na Simba.

Ni jambo la kusikitisha lakini Tanzania yetu ndivyo ilivyo, watu hawajutii wakiwa na kitu bali hujutia wakikosa kitu, nina imani siku moja viongozi waliosababisha ACACIA kujitoa watajutia tamaa zao ambazo leo ndiyo cha ya Liewig kuondoka na baadae Stand itakapoyumba bila shaka watamkumbuka sana kocha huyu.

Hakuna asiyefahamu misimamo ya Liewig katika kusimamia nidhamu, kuwajenga wachezaji na kuinua vipaji vya wachezaji nasikitika kumuona Liewing akiondoka wakati timu hiyo ikiwa kwenye ubora.

Comments