Simba: Mpeni muda Blagnon.


Kumeanza kuwa na uvumi kuhusiana na ubora wa mshambuliaji wa Simba Fredrick Blagnon aliyesajiliwa na timu hiyo kwa dau la milioni 100 za Kitanzania. Wapenzi wengi wa soka wameanza kuhoji ubora wa mshambuliaji ambaye amefunga bao moja pekee kwenye ligi kuu.

Jambo hili si kwa Blagnon pekee linamuhusisha na mshambuliaji wa Yanga Obrei Chirwa ambaye bado hajaonesha uwezo wake kwa wana jangwani hao licha ya kusajiliwa kwa dau nono la milioni 100 za kitanzania.

Sidhani kama mashabiki wanapaswa kufika huko kwa wakati huu nadhani watakiwa kumpa muda Blagnon, hadi sasa ni mechi 7 pekee zimechezwa kwenye ligi kuu bado anastahili kupewa muda, lakini pia Blagnon amekuwa akitokea benchi pengine amekosa muda mwingi wa kudhihirisha ubora wake kama ilivyo kwa Laudit Mavugo.

Nadhani na mazingira yanachangia, binafsi naona kama ligi ya Tanzania ina ugumu wake kwa wachezaji wa kigeni, bado ana nafasi kudhihirisha ubora wake, pengine akipewa nafasi ya kuzoea mazingira ya ligi anaweza kujiamini na kufanya vizuri na kuwapa kile ambacho wana Simba wanategemea.

Binafsi naona Obrei Chirwa wa Yanga alipata nafasi kubwa kuliko Blagnon nadhani wana soka na wapenzi wa Simba wampe muda Blagnon. Imewahi kuwa hivyo kwa mshambuliaji wa Liverpool Roberto Firmino ambaye hakufanya vizuri wakati ule wa Brendan Rodgers lakini sasa amekuwa moto chini ya kocha Jurgen Klopp.

Binafsi namuona Blagnon ni mchezaji ambaye anaweza kupata nafasi, bila shaka anafahamu kukaa kwenye eneo ambalo anatakiwa kupata nafasi ya kufunga magoli, kama mwalimu atabadilisha mawazo na kumwanzisha Blagnon kwenye baadhi ya mechi huenda akaonesha uwezo wake.

Imani yangu inaniambia kuwa kama Blagnon angekuwa amesajiliwa Yanga huenda angekuwa na idadi ya goli ambazo hazishuki tatu. Tatizo ni kuwa Simba haitumii mipira ya krosi hasa zile za juu kama ilivyo kwa Yanga ambao wana winga asilia kama Simon Msuva, Deus Kaseke ambao wamekuwa wakitumia mipira mirefu kumchungulia Hamis Tambwe pamoja na Donald Ngoma.

Mpeni muda Fredrick Blagnon nadhani anacho kitu katika soka huenda akipata nafasi zaidi basi mashabiki wa na wapenzi wa Simba watamwelewa.


Comments