May 24, 2017
Aliyekuwa kocha wa Crystal Palace Sam Allardyce ameachana rasmi na mpango wa kufundisha soka baada kujiuzulu Crystal Palace.
Sam mwenye miaka 62 ametangaza uamuzi huo baada ya kuinyanyua Crystal Palace kutoka nafasi ya 17 hadi 14 kwenye msimamo wa ligi ya England.
Sam alisaini miaka miwili na nusu ya kuinoa Palace baada ya kuchukua mikoba ya aliyekuwa kocha wa timu hiyo hapo awali Alan Pardew ambaye aliondolewa.
"Nimechukua uamuzi mgumu sana maishani mwangu, ingawa kuna watu wanaweza kufikiri ni jambo rahisi.
"Wakati huu nastahili kupumzika na wala sitajihusisha tena na soka ikiwemo kupokea ofa kutoka kwa timu yoyote ile.
" Ninamshukuru sana mmliki wa timu hii Steve Parish ambaye alirejesha hadhi na heshima yangu muda baada ya kuondolewa kuinoa England.
"Nadhani wote mnajua ni kipindi gani kigumu nilichopitia hapa, nafikiri imetosha, sitapokea ofa yoyote sasa." Alisema Sam.
Raia huyo amewahi kuzifua timu nyingi katika ligi ya England ikiwemo Bolton Wanderers, Sunderland, Blackpool, Huddlesfield, Blackburn Rovers, West Ham, kikosi cha England na Crystal Palace.

Comments
Post a Comment