Ndanda yaja na siku yao kama Simba.


Timu ya Ndanda FC ya Mtwara imefuata nyayo za Simba SC baada ya kuamua kuweka siku maalumu itayoitwa "Ndanda day" kwa mujibu wa Afisa habari wa timu hiyo Idrisa Bandari.

Tamasha hilo litafanyika leo Agosti 20, katika uwanja wa Chamanzi Complex ambapo pia kutakuwa na utambulisho wa wachezaji wapya pamoja na mchezo wa kirafiki dhidi ya Ruvu Shooting.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Masoko wa Ndanda FC Peter Simon amesema kuwa wamejiridhisha na utafiti walioufanya na wamebaini kuwa mbali na Mtwara timu hiyo ina mashabiki Dar es Salaam hasa katika maeneo ya Mbagala na Temeke.

"Baada ya kufanya utafiti tumegundua kuwa tuna mashabiki wengi Dar es Salaam hasa katika maeneo ya Temeke na mbagala na ndiyo maana tumeleta sherehe hizi Chamanzi." Alisema Simon

Ndanda watafanya tamasha hilo pia katika mkoa wa Mtwara kwenye makao ya timu hiyo katika siku ya ufunguzi wa ligi Vodacom watakapochuana na Azam FC.

Pia tamasha hilo litashirikisha wasanii wa bongo Fleva ambao watasherehesha sherehe hizo akiwemo Jay Me, TID na Juma Nature ambao wote ana asili ya Mtwara.

Comments