Naikumbuka fainali ya mwaka 2009 ya Uefa Champions League (UCL), Barcelona walitoa adhabu kwa kuichapa Manchester United mabao 2-0. Katika mchezo huo
Barcelona ilimkosa beki wake muhimu Dani Alves ambaye alikuwa na Adhabu ya kadi mbili za njano.
Kwa jinsi Barcelona walivyokuwa imara usingehisi kama Alves hakuwepo kikosini, na Mkongwe Carles Puyol alisimama vyema upande wa kulia, ushirikiano ulikuwa wa hali ya huu hakuna ambaye angeweza kupinga jinsi Barcelona walivyokuwa bora kipindi kile.
Najaribu kuingalia Barcelona kwa sasa imepoteza ubora wake na Real Madrid wanaonekana kama ni wakati wao kwa sasa tangu Zinedine Zidane alipotia maguu na kuchukua mikoba ya Rafael Benitez January mwaka jana.
Wakati ule Iniesta alikuwa bora, Xavi bora zaidi na hata kijana mdogo Sergio Busquets alionekana kuitendea haki sehemu kiungo.
Tangu mwaka jana Lionel Messi alionekana hakubaliani na vile timu ilivyokuwa inaenda chini ya Luis Enrique ambaye aliitengeneza vema mchanganyiko wa Messi, Suarez na Neymar (MSN) na kumlaumu kocha huyo kushindwa kutafuta mbadala wa Dani Alves pamoja na Xavi Hernandez.
Namuunga mkono Messi katika eneo la kiungo, ingawa pia Sergi Roberto aliruhusu magoli mengi upande kulia na kuigharimu Barcelona msimu uliopita.
Adui mkubwa wa Barcelona ni kiungo na ndiyo eneo sahihi ambalo kiujumla limepoteza msisimko na mvuto katika timu ya Barcelona. Nikianza Sergio Busquets ni wazi amechoka majeraha ya mara kuwa mara na pia ametumika kwa muda mrefu bila kupata mbadala wake kwenye kikosi, ingawa Denis Suarez alirejea kwa mara nyingine Barcelona lakini ameshindwa kuyabeba majukumu ya Busquets ipasavyo.
Nina imani hata MSN ingebaki kwa msimu huu unaonza kama Barcelona itashindwa kutibu eneo la kiungo wasitegemee mabadiliko.
Binafsi nampenda sana kocha aliyeachia ngazi Barca Luis Enrique ila namlaumu alishindwa kucheza na alama za nyakati mapema, ni wazi aligundua umri wakina Iniesta na Busquets unaenda alishindwa kulenga watu sahihi ambao huenda kwa sasa wangekuwa msaada kwenye timu.
Bado Barcelona ina wakati mgumu sana kurekebisha eneo la kiungo ingawa kwa sasa wamemsajili Paulinho huwez kuweka asilimia mia kuwa anaweza kufanya vizuri ingawa kuna aina ya kiungo ukimtazama hata kwa haraka bila shaka unaweza kusema anafaa kuwa Barcelona.
Lakini naiona Barcelona imechelewa kwa sasa kuondoka Blaise Matuidi ambaye anajiunga na Juventus jibu litakuwa wazi kuwa PSG hawatakuwa na mpango wa kumuachia kiungo Marco Veratti, na mwaka jana walijisikilizia sana kufanya maamuzi na hatimaye Pogba alitua Manchester United.
Wafungaji wa magoli katika ligi ya Premiera Liga walitoka Barcelona hii inaonesha wazi Bado timu hiyo ina makali eneo la mbele lakini katikati kimebaki kitendawili.
Najiuliza kuwa Phelipe Coutinho anaweza kuwa mrithi sahihi wa Neymar kama inavyodhaniwa lakini, je mfumo wa kiungo ukiendelea kuzorota Barcelona itaweza kuwika au itashia kuangukia pua kama ambavyo imechemsha kwa Real Madrid katika mechi ya Super Copa 2017.
Ninahisi Zinade ana akili na taratibu ameanza kuisoma Barcelona na amefahamu ni sehemu gani atawanasa, katika mchezo wa jana Zidane aliwatupa benchi Gareth Bale na Isco pia Ronaldo hakuwepo kwa sababu alifungiwa lakini aliweza kuifunga Barcelona bao 2-0 na kutimiza idadi ya magoli matano.
Kuna kitu watu bado wanasahu enzi za Gurdiola alikuwa haofii kuwaweka vijana wadogo kama Christian Tello, Isaac Cuenca na Pedro Rodriquez katika eneo la pembeni wakiongozwa na kaka yao Messi ni kwa sababu alishajua ni wakina waliobeba timu kwanza kabla hawajafika kwenye nyavu za wapinzani.
Alijiamini na kina Xavi Hernandez, Sergio Busquets na Andres Iniesta hasa eneo la Xavi ambalo bila shaka lilitengeneza mamia ya pasi uwanjani, na ndiyo jeuri ya zidane ilipo sasa, bila shaka anajivunia Casemiro au Mateo Covacic, Tony Kroos, Luka Madric au Isco kisha anawaamini vijana wadogo kama Marco Asensio ambao wanafanya maajabu hata kama wakina Ronaldo na Bale wapo.
Barcelona imemsajili Nelson Semedo kutoka Benifica pamoja na Douglas kutoka Deportivo la Coruna wote hawa ni mabeki wa kulia naweza kucheza kamali huenda wakachemsha kama eneo la katikati litashindwa kuwa Imara.
Ni kama Dani Alves alisoma mazingira na kuamua kwenda kumpumzika kwenye timu nyingine ni wazi eneo la kiungo lisingempa Uhuru kama hapo awali wakina Xavi, Iniesta na Busquets walipokuwa kwenye ubora.
Beki wa Barcelona Gerard Pique amekubali kwa mara ya kwanza timu yake imekuwa dhaifu mbele ya Real Madrid katika kipindi cha miaka 9 alipokuwa ni jambo ambalo linaonekana dhahiri kwa kwa sasa, kama hawatajipanga itakuwa ngumu kumdhibiti Zidane.
Pique akisikitika
Huu ni mtazamo wangu, nina imani kuwa Coutinho na Ousman Dembele ambaye ana dalili zote kutua Barcelona wanaweza kupeleka mabadiliko ya 50℅ lakini zilizobaki eneo la kiungo katika timu hiyo litaamua.




Comments
Post a Comment