Nyuma ya pazia Mayanja anamkosoa Omog kiaina.


Wikiendi hii mechi mbali mbali za ligi kuu Tanzania Bara zilichezwa katika viwanja tofauti na moja kati ya mechi hizo ni ile ya Simba na Azam ambayo ilimalizika kwa sare isiyokuwa na magoli pale Chamanzi Complex.

Si mara ya kwanza kumsikia msaidizi wa kocha wa Joseph Omog, Jackson Mayanja akihuzunishwa na udhaifu wa umaliziaji katika safu ya mbele ya wekundu hao. Sitaki kuamini hata kwangu Binafsi timu iliyopata ushindi wa mabao 7-0 ilikosa hata bao moja pale Chamanzi.

Katika hili liko wazi kuwa Joseph Omog ni mwalimu na mwenye mbinu nyingi za kiufundi na mafaniko yake yako wazi. Ndani ya nchi yetu kocha huyo amewahi kuipa Ubingwa Azam FC pamoja kuipatia Simba taji la kombe la FA.

Azam imekuwa kipimo tosha wa Simba ambayo ilijigamba baada ya kufanya usajili mkubwa msimu huu. Ingawa Okwi na Luizio ambao walifanya balaa katika mechi ya kwanza hawakuwepo lakini nina bado Simba ingeweza kufanya vizuri kutoka na uwepo wa washambuliaji walio bora kwenye kikosi chao kama Nicholas Gyan, John Bocco, Ludit Mavugo, Mohamed Ibrahim na Shiza kichuya.

Niliwahi kuandika makala yangu ya kwanza, kuwa endapo Omog atashindwa kushambulia atakuwa kwenye wakati mgumu kutokana na matarajio ya Simba yalivyo makubwa msimu huu. Hali hiyo imechangiwa na usajili mkubwa ambao umefanywa na Simba kulinganisha na klabu nyingine yoyote nchini.

Simba ambayo ilipata timu iliyo imara hapo jana ilishidwa kuonesha makali katika eneo la ushambulizi licha ya kutawala zaidi eneo la kati hasa katika kipindi cha pili hali iliyopelekea kupoteza pointi 2 muhimu baada ya kugawana pointi moja na wenyeji.

Kitendo cha Mayanja kulalamikia jambo moja kila wakati ni kiashiria kuwa Simba imeshindwa kuboresha eneo hilo. Kwa Lugha rahisi ni kwamba Omog ndiye kinara katika benchi la ufundi la Simba ni lazima lawama zitakuwa kwake.

Ni jambo lililowazi kuwa Simba ilichemsha kumzuia Yanga kutetea ubingwa kutokana na fowadi isiyokuwa na uchu wa mabao licha kufungana kwa pointi 68 na mtani wake lakini Yanga iliweza kuwa Bingwa mbele ya Simba.

Wakati wote kocha wa Simba amejitahidi kuunda safu imara ya ulinzi na kiungo, hapana shaka juu ya hilo kuwa Simba wapo imara zaidi katika eneo la kiungo kulinganisha na timu yoyote kwa sasa kwenye ligi ya Tanzania.

Ingawa Mayanja ni msaidizi wa kocha Joseph Omog lakini inambidi kutoa ya moyoni kwenye mahojiano na wana habari kama sehemu ya kuongeza changamoto kwa bosi wake huyo, ili kuboresha mbinu za kiufundi katika fowadi ya Simba.

Kwa wadau wa soka na wapenzi wa Simba ambao wanatilia shaka tatizo hilo katika timu yao ni wazi kuwa Mayanja anapalia makaa ya moto kuwa tatizo hilo linaigharimu Simba kwa asilimia kubwa ingawa kama kocha ana nafasi ya kuzungumzia masuala ya kiufundi.

Simba inatakiwa kuonesha mabadiliko, kuwa wamebadilika ikilinganishwa na matokeo waliyopata kwenye msimu uliopita, kwa kufuta makosa yao na kufanya mambo yenye kushangaza ili wadau na wapenzi wa soka tumsikie akizungumzia mambo mengine na kusifia ubora wa eneo ambalo ni jitihada za kocha mkuu Joseph Omog.


Comments