Siri za Biblia: Nani alisema na wewe utashindwa, usihukumiwe na historia


Leo natamani kukutia moyo katika mambo yako, juhudi zako na mipango yako, kazi zako, na katika ile njia ya kumtumikia Bwana wala usiogope.

Kuna watu wanaamini wanaweza kuyashika maisha ya watu mikononi. Au anaweza kuhukumiwa na historia. Inawezekana kuna ndugu yako biashara zake zilikufa na wewe unaogopa kufungua biashara yako, unaogopa kuanguka. Pengine wazazi walizama kwa usafiri wa meli nawe waogopa kutumia meli kwenye safari zako. Basi leo nakwambia usiogope. 

Nataka nikwambie siku hazilingani, hatma ya Frank siyo ya John, songa mbele, Kama kuna watumishi walikufa kwa kuitetea injili wala usirudi nyuma endelea kuthubutu kwa sababu ipo habari njema juu yako.

Matendo (12:2) "Akamwua Yakobo, ndugu yake Yohana kwa upanga." 

Maandiko yanatueleza kwamba baada ya kifo cha Yakobo nduguye Yohana jambo hilo lilipendeza mbele ya wayahudi na Herode hali akitaka sifa alimkamata na Petro akamweka ndani.

Maandiko yanaeleza kanisa lilikesha, Petro alikombolewa na malaika wa Bwana akamtoa na kumwongoza hadi mahali palipo salama.

Herode alisahau ya kwamba siku hazilingani. Na Mungu alikuwa ameamua vinginevyo kuhusu Petro. Hata kanisa halikuamini walipomwona Petro amerudi akiwa hai. 

Walijua kifo kitamkuta Petro kama ilivyokuwa kwa Yakobo

Kama kuna mwovu nyuma yako, au Jambo lenye kutia hofu mkabidhi Bwana kwa bidii kama ambavyo kanisa lilimwomba Bwana kwa juhudi (Matendo 12:5)

Usiogope maana wenye hila kama Herode Bwana hubadili hatma zao ili wewe usiumie, soma Matendo 12:23,

Fikiria tu laana aliyojizoleaa Yezebeli kwa kuua manabii wa Mungu. Vipi kuhusu Hamani alipotaka kumuua Mordekai kwa kutumia cheo na madaraka kwa hila zake binafsi. Maandiko yanatueleza Esta, Mordekai na wayahudi walifunga siku tatu kavu na kuomba kwa juhudi, habari njema ni kwamba usiku ule mfalme Ahasuero hakulala (Esta 6:1). Hii ndiyo nguvu ya maombi pale unapoamua kuomba kwa juhudi. 

Jambo jema kwa mwanadamu ni kumkabidhi Bwana hatma yako, wewe muombe kwa bidii tena bila kuchoka na endelea kumshukuru kwa mema yote kila siku. Maombi ni silaha ya mabadiliko katika maisha ya mwanadamu. Maombi hubadili historia, maombi hubadili laana kuwa baraka, kifo kuwa uzima, hata vilivyokufa hufufuka kupitia maombi.

Basi kuanzia leo 


Usiogope kuthubutu; 

1. Ishi ndoto zako

2. Inua biashara zako 

3. Simamia ndoa yako

4. Pambania maono yako 

5. Usiogope kwa sababu wengine walishindwa 

6. Endelea kuthubutu na itumie kila fursa 

7. Amini katika Mipango yako 💪🏽

Usihukumiwe na historia, amini tu hata kama huna urafiki na matajiri lakini siku moja unaweza kuwa Rais au nafasi yoyote ile katika uongozi wa juu.

Imeandaliwa; 

Student wa Bible Class 

Kapinga Jr

Email:kapingaemanuel@gmail.com 

0718143834

Comments

Post a Comment