Nani anayesema wewe siyo Mfalme au Rais.

 

Usiogope! Umeumbwa kwa kusudi la Mungu. Una thamani sana.

Key Line/Mstari mkuu 2 Samweli 7:8

Inashangaza sana, pale ambapo kuna watu hujishusha na kuamini wengine wana thamani kuliko wao 

Bado yupo mtu anaamini kwa sababu yeye alizaliwa kijijini, alipitia maisha ya umaskini na shida basi hawezi kuwa mtu wa nafasi fulani siku moja, pengine Rais au Waziri au kiongozi wa nafasi yoyote katika nchi hii. Wapo waliozaliwa nje ya ndoa, wengine kutokana na sababu za uzinzi na uasherati, nakwambia hakuna siku Bwana amekuacha labda wewe mwenyewe uamue kumuacha.

Mimi ni nani? Ni mtoto wa Mungu. Je nina thamani? Ndiyo kwa sababu Bwana ananijua. Maandiko yanatueleza  

"Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa." Yeremia 1:5 

Wakati Yeremia akijiona hastahili nafasi aliyopewa na Mungu, BWANA anamwambia amemfanya kuwa nabii wa mataifa.

Kwanini wewe uogope? Kama una kitu, una ujasiri, una maono, na wito unawaka ndani yako songa mbele maana Bwana aliendelea kumwambia Yeremia

"Usiogope kwa sababu ya hao, maana mimi ni pamoja nawe nikuokoe..." Yeremia 1:8

Kama Bwana alisema wewe ni Rais au Waziri, usiogope maana atakayekuokoa ni yeye, katika misuko suko, tabu na nyakati ngumu atakuwa na wewe.

Kamwe thamani yako haipatikani kwa sababu ulizaliwa Ikulu, au wewe ni binti au kijana wa tajiri namba moja duniani au niwe mjukuu wa familia za kifalme Kama uingereza kwa Malkia Elizabeth au kule Eswatini kwa King Mswati bali kwa kusudi la Bwana peke yake.


Uzinzi wa Daudi na Bathsheba haukumfanya Bwana asimpende Sulemani. Huenda Bathsheba alikuwa mlezi bora wa mfalme Daudi kuliko wake wengine wa mfalme. Bado kusudi la Mungu lilikuwepo.


"Naye Daudi akamfariji Bathsheba mkewe, akaingia kwake, akalala naye; naye akazaa mwana, akamwita jina lake Sulemani. Naye Bwana akampenda." 2Samwel 12:24 

Bwana hakuacha kumpenda Sulemani kwa sababu alizaliwa kupitia mke wa Uria, aliyekuwa kama mchepuko kwa Daudi.  Tambua kwamba Mungu anakupenda na ameweka Lulu ndani yako.

Na Sulemani akawa mfalme mkubwa, tajiri, maarufu na mwenye hekima sana akiheshimisha kiti cha baba yake Daudi.


Haijalishi ulizaliwa na wazazi wa namna gani, jambazi, kahaba, au muuaji bado lipo kusudi la kuzaliwa kwako.


Yeftha alitupwa na ndugu zake, hakupewa hata sehemu ya urithi na ndugu zake kwa sababu alizaliwa na mwanamke kahaba lakini alifanyika kuwa mwamuzi wa Israel kwa miaka 6. Na jina lake limeandikwa Kati ya mashujaa walioitetea Israel mpaka leo.


"Basi huyo Yeftha, Mgileadi, alikuwa mtu shujaa sana, naye alikuwa ni mwana wa mwanamke kahaba; Gileadi akamzaa Yeftha." Waamuzi 11:1 


Kamwe usijidharau, amini wewe unaweza, una nafasi ya kuwa shujaa na kufanya makubwa duniani. Mfalme Daudi alijiona yeye ni mchunga kondoo tu, tena hakupewa hata nafasi ya kwenda vitani kama kaka zake lakini machoni pa Bwana alikuwa mfalme mwenye kulijenga taifa lake.


Katika nafasi ya chini uliyo nayo hakika BWANA anakuona katika nafasi nyingine 


"Basi sasa, mwambie mtumishi wangu, Daudi, maneno haya, BWANA wa majeshi asema hivi, Nalikutwaa katika zizi la kondoo katika kuwaandaa kondoo, ili uwe mkuu juu ya watu wangu." 2Samwel 7:8 

Ikiwa Bwana alimuinua Daudi ambaye alizaliwa nje ya ndoa, na kumfanya mfalme, hakuwa amesoma wala kuwa na wasifu mkubwa wa kisomi, ataachaje kukuinua na wewe.

Acha kuzika maisha yako, ndoto zako wala wewe siyo mnyonge mbele ya kusudi la BWANA 


Yupo binti mmoja alienda kanisani, akamlilia Bwana na kuomba kwa bidii kwamba ndoto yake kubwa ni kuolewa na Rais. Alianza mahusiano na tajiri wa kwanza wakashindwana akaja tajiri wa pili pia ya mahusiano yakashindikana.


Ghafla alikuja msomi wa sheria maskini ambaye wazazi wake hawakumwelewa na binti alichukua uamuzi wa kuolewa nae. Ingawa wazazi wa binti walipata huzuni wakidhani binti yao alichezea nafasi ya kuolewa na matajiri.


Miaka ilisonga yule mwanasheria alipewa nafasi agombee kinyang'anyiro cha urais, akiwa anajiona wa kawaida kila mmoja alielewa sera zake hatimaye yule mwanasheria alishinda urais na binti alibahatika kuwa first Lady kama ambavyo alimuomba Mungu huko nyuma. Binti anaitwa Marry Todd aliyekuwa mke wa Rais maarufu wa Marekani Abraham Lincoln ambaye aliweka historia ya kuwa rais wa 16 wa taifa kubwa la Marekani. 


Ingekuwaje Kama Mary Todd angeolewa na yule tajiri, huenda ndoto yake isingetimia, lakini aligundua hitaji lake kwa mwanasheria maskini, huenda Mungu alimjaribu katika hilo na alishinda mtihani wa ombi lake. Mary Todd aliona thamani ya Lincoln kwa jicho la maono halisi kitu ambacho hakikuwepo kwa wale matajiri.


Usiogope, vaa ujasiri na ushinde uwoga, kwa maana thamani ya mwanadamu inahitaji bidii, uvivu ni adui anayewaponza wengi ulimwenguni 


"Na huyo Yeroboamu alikuwa mtu hodari, shujaa; Sulemani akaona ya kuwa kijana huyo ni mtu mwenye bidii akamweka juu ya kazi yote ya nyumba ya Yusufu." 2Falme 11:28


Mpende Mungu, lilia baraka zake na wala usimpe mpaka wa mafanikio yako kama ambavyo yabesi alifanya (1Nyakati 4:10). Huenda ana kusudi la kukufanya taifa kubwa zaidi kuliko ambavyo wewe unafikiri.

Badala ya kujiona umekosa thamani, wewe kazana kupambana omba kubarikiwa.

Imeandiliwa;

Student wa Bible Class 

Kapinga Jr, 0718143834, kapingaemanuel@gmail.com 

Comments