Sehemu ya pili
Unawezaje kuhusiana na Mungu bila Roho? Ukweli ni kwamba haiwezekani. Hatuwezi kuhusiana na Mungu kwa jinsi ya mwili bali Roho; Mungu alipoamua kumuonyesha Ezekiel maovu wafanyayo wazee wa Israel gizani wala haikuwa kwa jinsi ya mwili bali Roho, maana roho ndiyo iliyomuinua ma si mwili.
"Naye akanyosha mfano wa mkono, akanishika kwa kishungi kimoja cha nywele za kichwa changu; nayo roho ikaniinua kati ya dunia na mbingu, ikanileta katika maono ya Mungu mpaka Yerusalemu, mpaka mlango wa kuingilia ua wa ndani uelekeao upande wa kaskazini; mahali palipokuwa pamewekwa sanamu ya wivu, itiayo wivu. 4 Na tazama, huo utukufu wa Mungu wa Israeli ulikuwapo hapo, sawasawa na maono yale niliyoyaona katika bonde." Ezekiel
Kabla ya kuondoka kwa Yesu Kristo aliahidi kuleta msaidizi atakayetuongoza kusimama sawa sawa na kusudi la Mungu. Yesu mwenye alisema;
"Nami nitamwomba Baba, naye atawapa msaidizi mwingine, ili akae nanyi hata milele..." Yohana 14:16
"Yeye atanitukuza mimi, kwa kuwa atatwaa katika yaliyo yangu ili kuwapasha habari." Yohane 16:14
Mpendwa kama ulivyomsikia YESU mwenyewe, hatuwezi kujua kusudi lake, hata habari zake kama hatuna huyu msaidizi ambaye alimleta kwetu ili tusibaki yatima.
Lakini ana masharti yake, ili umpokee huyu msaidizi ni lazma ukubali kuwa mwana wa Mungu, hakuna namna nyingine vinginevyo utakuwa unatwanga maji kwenye kinu.
"Bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika wana Mungu, ndiyo wale waliaminio jina lake." Yohana 1:12
Ndugu yangu kama hujampokea YESU KRISTO na kuliamini jina lake kuwa ndiye Bwana na mwokozi wa maisha yako, basi utapoteza haki ya kuwa mwana wa Mungu. Utapoteza kibali cha kuhusiana na Mungu kwenye maisha yako kwa kuwa Mungu anahusiana na mwanadamu kwa jinsi ya roho. Mtume Paulo anasema hao wenye kuongozwa na roho wa MUNGU ndiyo wana wa MUNGU (Rumi 8:14). Hakuna namna nyingine.
Ili kuzifahamu siri za mbingu na kupokea mafunuo ya Mungu katika maisha yetu tunamuhitaji Roho Mtakatifu, kwa nguvu zetu, akili zetu, elimu yetu wala hatuwezi bali kupitia Roho Mtakatifu; "Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu."
Siku za leo kuna madhehebu mengi na makanisa mengi sana huchanga michango mingi na mikubwa ili kujenga makanisa makubwa na ya kifahari, lakini ndani yao BWANA hayupo wala makanisa yao hayaongozwi na roho. Je Mungu anahitaji yote hayo?
Yesu aliwahi kuwaambia wayahudi; "...livunjeni hekalu hili nami katika siku tatu nitalisimamisha." Yohana 2:19. Ajabu ni kwamba hawakumuelewa Yesu na yapo makanisa na madhehebu mengi huenda hawamwelewi Yesu mpaka.
Makanisa makubwa na nyumba za ibada za gharama hazina maana kwa Mungu ikiwa waumini wa makanisa wamekufa kiroho, ikiwa Yesu hayupo ndani yao, wala hawajampokea Roho au kuongozwa naye.
Yupo mtumishi mmoja wa Mungu alisikia sauti ya BWANA ndotoni ikimwambia, majengo makubwa wajengayo na hayo makanisa hayana maana ikiwa watu wake wamekufa kiroho. Wala hayataki
Ikiwa watu wanajenga makanisa ya gharama lakini YESU hayupo kwenye maisha ya waumini, wanakuwa hawana tofauti na wale wayahudi ambao hawakumwelewa YESU juu ya habari ya ujenzi wa hekalu kwa siku tatu. Maana Yesu alizungumzia kazi ya msalaba uletao wokovu kwa watu wote.
Injili za uchumi na kutiana moyo kwenye mambo yasiyo na msingi kiroho zimepewa kipao mbele siku za leo huku roho za waamini zikiteketea ukosefu wa kweli ya Mungu.
YESU alifanya kazi kubwa msalabani kwa ajili yako na Yangu, alifanyika sadaka iliyokuu, dhabihu ya ukombozi kwa ajili yako na yangu mpendwa. Kazi imebaki kwako na kwangu kumtengenezea Mungu hekalu alitakalo mahali pa waabudio halisi.
Watu wengi leo hawaoni utendaji wa nguvu za Mungu ndani yao, kwa sababu hawajatengeneza madhabahu iliyosafi kwa ajili ya Bwana kufanya makao. Hatujaweka daraja zuri la kuhusiana na Roho wa MUNGU.
YESU mwenyewe katika maandiko anatukumbusha kuwa hakuna aliye mtakatifu kama MUNGU wa mbingu. Ikiwa Mungu ni Mtakatifu basi huusiana na vilivyo vitakatifu.
Tukipokea haki ya kuwa wana, ndiyo mwanzo mpya sisi kuenenda katika utakatifu kwa kuwa MUNGU ni Mtakatifu. Tuliona kuwa wale waongozwao na Roho Mtakatifu ndiyo wana wa Mungu.
Daudi alishuhudiwa na Roho wa Bwana kuwa roho ya Mungu ipo kila mahali;
Zab 139:7-10
Niende wapi nijiepushe na roho yako? Niende wapi niukimbie uso wako? Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko; Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko. Ningezitwaa mbawa za asubuhi, Na kukaa pande za mwisho za bahari; Huko nako mkono wako utaniongoza, Na mkono wako wa kuume utanishika.
Ukweli pamoja na kuwa Roho ya Mungu ipo kila mahali lakini huchagua mahali pa kukaa. Roho ya Mungu hukaa mahali gani?
"........Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo ya waliotubu." Isaya 57:15b
Tazama Roho ya MUNGU yakaa patakatifu pamoja na wale waliotubu. Hivyo hatuwezi kuwa na nguvu za Mungu ndani yetu, wala hatuwezi kupokea utendaji wa Roho Mtakatifu ikiwa tumeichagua dunia na kumpa Mungu kisogo kwa matendo yetu maovu.
Kama ambavyo MUNGU kwa pendo lake aliachilia wokovu kwa watu wote na mataifa (Yohana 3:16-17), kadhalika ameziachilia nguvu zake ili kila aendaye kwa uadilifu na utakatifu azipokee.
"Kwa maana macho ya Bwana hukimbia-kimbia duniani mwote, ili ajionyeshe mwenye nguvu kwa ajili ya hao, waliokamilika moyo kuelekea kwake. Kwa hayo umetenda upumbavu; kwani tangu sasa utakuwa na vita." 2 Nyakati za 16:9
Mungu ametupendelea mno wanadamu. Tatizo ni mioyo yetu tumeizuia kuelekea kwake. Hatutaweza kumuona, wala kuzipokea nguvu zake ikiwa hatutengeneza mioyo yetu kumuelekea yeye." Maana wale wenye mioyo safi ndiyo watamuona Bwana (Mathayo 5:8), na wataziona nguvu zake pia.
Ndiyo maana Paulo anatukumbusha kuwa yatupasa kuenenda kama wana nuru maana tumeondoka katika giza la dhambi, tangu tulipokubali kumpokea Yesu awe Bwana na mwokozi wa maisha yetu.
"Kwa maana zamani ninyi mlikuwa giza, bali sasa mmekuwa wa nuru katika Bwana; enendeni kama watoto wa nuru." Efeso 5:8
Kama ambavyo giza na nuru haviwezi kukaa pamoja, ndivyo Roho ya MUNGU isiyoweza kufanya USHIRIKA pamoja na ile roho isiyotubu, roho iliyojaa uovu na uasi ndani yake.
Makanisa mazuri na ya kisasa hayana maana kwa Mungu ikiwa watu wake roho zao zimekufa katika dhambi. Kwa kufa kwake Bwana YESU pale msalabani alitufanya sisi kuwa hekalu mbele ya majengo mazuri, na ndani yetu imewekwa madhabahu ya upatanisho yaani roho, kadili madhababu ilivyo safi na kuepuka unajisi na ndiyo Bwana anavyozidi kusogea kutengeneza madhabahu imara yenye kumuunganisha Mwanadamu na roho yake.
Siri hii ilifichuliwa kwetu kupitia maandiko. Mtume Paulo alisema;
"Au hamjui kuwa miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, mliyepewa na Mungu? Maana mlinunuliwa kwa thamani sana. Basi sasa mtukuzeni Mungu katika miili yenu." 1 Kor 6:19-20
Haleluya, Bwana Yesu asifiwe, Bwana Yesu apewe sifa, maana alitununua kwa thamani sana kwa njia ya msalaba. Kama ambavyo Paulo alisema na kanisa la Korintho, Yesu anastahili kutukuzwa kwa miili yetu. Huu ni wakati wa kukimbia uongo, uzinzi na uasherati, anasa za dunia, ibada za sanamu na mambo yote ya uasi.
Anza leo kuisikia sauti ya Bwana rohoni mwako, hakuna namna nyingine ya Kuhusiana na MUNGU aliye hai kwa jinsi ya mwili bali roho na ndipo atafanya madhabahu ndani yako. Fanya maamuzi leo, mpokee YESU awe Bwana na mwokozi wa maisha yako, kiri kwa kinywa chako, akupe roho mtakatifu atakayekuongoza katika yote kuanzia leo. Na Roho ya Bwana itaenenda na wewe kila mahali maana ni ahadi yake (Hagai 2:5). Wala usiogope
Mungu akubariki sana kwa Muda wako
Imeandaliwa;
Kapinga Jr
Student of Bible Class
0718143834
kapingaemanuel@gmail.com
.jpeg)
Comments
Post a Comment