Ukisoma kitabu cha Mwanzo sura ya 1:26 maandiko yanasema; "Mungu akasema, na tumfanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu..."
Hivi ni kweli, sisi tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu kwa namna gani? Kwani Mungu ni nani? Maandiko yanasema MUNGU ni roho. Ikiwa Mungu ni roho basi mahusiano kati ya Mungu na mwanadamu hayapo kwa jinsi ya mwili bali roho.
Ukisoma kitabu cha Ayubu 33:4 maandiko yanazidi kuthibitisha kwamba mwanadamu aliyeumbwa na Mungu amekamilishwa kuishi na kupokea uhai kwa jinsi ya roho
"Roho ya Bwana imeniumba Na pumzi za Mwenyezi hunipa uhai." Hivyo tumepata majibu kwamba mashine ya mwili wa binadamu ni roho, ndiyo maana mtu anapokufa tunabaki na mwili tupu usiosikia wala kutikisika.
Hata gari iwe na body mpya nzuri kiasi cha kuvutia kila mmoja anayeitazama lakini bila engine (mashine) imepoteza maana, ipo hivyo kwa mwanadamu pia mwili hauna maana bila roho.
Kama MUNGU angekuwa kwa jinsi ya mwili basi bila shaka tungewasiliana Naye kwa jinsi ya mwili lakini Yeye ni roho, hivyo tunaweza kuwasiliana na Mungu kwa jinsi ya roho.
Mungu anajieleza mwenyewe katika maandiko kwamba Yeye ni "roho" (Yohana 4:24). Tazama anavyojidhihirisha katika ahadi yake kwa Waisrael;
"Kama neno lile nililoagana nanyi mlipotoka katika Nchi ya Misri; na roho yangu inakaa kati yenu msiogope." Hagai 2:5
Hivyo MUNGU anajidhirisha mwenyewe kwamba hawezi kuwa kati yetu kwa jinsi ya mwili bali roho. Jiulize utawezaje kuwasiliana na Mungu kwa jinsi ya mwili? Jibu lipo wazi kwamba haiwezekani. Kuna wakati tunamuomba Mungu mambo makuu kama ulinzi wake, inahitaji imani sana kuelewa kwamba Bwana anatulinda siku zote. Lakini bila macho ya rohoni, bila kuwa rohoni ni ngumu sana kuelewa jambo hili; tazama ilivyokuwa kwa Gehazi aliyekuwa mtumishi wa nabii Elisha
"15 Hata asubuhi na mapema mtumishi wake yule mtu wa Mungu alipoondoka, na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu, na farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi wake akamwambia, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyeje? 16 Akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao. 17 Elisha akaomba, akasema, Ee BWANA, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. BWANA akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote."
Unaweza kujionea, ilivyokuwa ngumu kwa Gehazi kutambua ulinzi wa BWANA kwa jinsi ya mwili lakini Elisha alimwomba MUNGU ampe macho ya rohoni aweze kuona.
Ipo wazi kwamba hatuwezi kuwasiliana na MUNGU wala kumwelewa kwa jinsi ya mwili bali roho. Ndiyo maana kupitia kinywa cha nabii Yoel Bwana aliahidi kuachilia uweza wa roho yake kwa wale wote wenye mwili yaani sisi
"28 Hata itakuwa, baada ya hayo, ya kwamba nitamimina roho yangu juu ya wote wenye mwili; na wana wenu, wa kiume na wa kike, watatabiri, wazee wenu wataota ndoto, na vijana wenu wataona maono; 29 tena juu ya watumishi wenu, wanaume kwa wanawake, katika siku zile, nitamimina roho yangu." Yoel 2:28-29
Bwana alijua bila uweza wa roho yake ingelikuwa ngumu kwa mwanadamu kuhusiana Naye, mwanadamu angetegemea kuisikia sauti ya Bwana kwa kinywa cha manabii wake milele. Lakini MUNGU anamtaka kila mmoja ahusiane Naye, maadamu una mwili naam Roho ya Bwana itakujilia.
Tena Bwana anaendelea kusema; "Nami nitaonyesha mambo ya ajabu katika mbingu na katika dunia, damu, na moto na minara ya moshi." Yoel 2:30
Hayo yote asemayo Bwana hayawezekani kwa jinsi ya mwili bali kwa jinsi ya roho. Ukiwa na Roho Mtakatifu hapo sasa unapokea rasmi haki ya kuhusiana na Mungu.
Kwa hiyo sasa tunaweza kuamini kwa pamoja kwamba kwa mfano na sura ya Mungu tuliyopewa sisi ni kwa jinsi ile ya roho na si mwili kama tunavyodhani. Kwa kuwa Yeye hana mwili bali MUNGU ni roho.
Itaendelea kesho.....
Imeandikwa na;
Student wa Darasa la Biblia
0718143834
kapingaemanuel@gmail.com
.jpeg)
Comments
Post a Comment