SIRI ZA BIBLIA: Je, unaabudu usichokijua



19 Yule mwanamke akamwambia, Bwana, naona ya kuwa u nabii! 20 Baba zetu waliabudu katika mlima huu, nanyi husema ya kwamba huko Yerusalemu ni mahali patupasapo kuabudia. 21 Yesu akamwambia, mama, unisaidiki, saa inakuja ambayo hamtamwabudu Baba katika mlima huu wala kule Yerusalemu. 22 Ninyi mnaabudu msichokijua lakini sisi tunaabudu; kwa kuwa wokovu watoka kwa wayahudi. 23 Lakini saa inakuja, nayo sasa ipo, ambayo waabuduo halisi watamwabudu Baba katika roho na kweli. Kwa maana Baba atafuta watu kama hao wapate kumwabudu. 


Maandiko yanasema Mungu ni roho. Hivyo kama unataka kumwabudu haitakuwa tena kwa jinsi ya mwili au vitu (mapambo, kazi za sanaa). 


Saa inakuja ambayo waabuduo halisi hawatahitaji kuwa mlimani wala Yerusalemu kwa jinsi ya mwili bali katika roho. Nasi tutaupanda mlima wa ukamilifu katika ukamilifu kwa jinsi ya roho. Ndipo Daudi anaposema; 


3 Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana? Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake? 


4 Mtu aliye na mikono safi, na moyo mweupe, asiyeinua nafsi yake kwa ubatili, Wala kuapa kwa hila 


5 Atapokea baraka kwa BWANA na haki ya Mungu kwa wokovu wake. 


6 Hiki ndicho kizazi cha wamfuatao, wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. Zaburi 24:3-6 


Unaweza kwenda kanisani kila jumapili na usijue kile unachokiabudu. Ukapoteza muda na wala usimuone Mungu. Kwa kuwa bado haujui kile unachokiabudu. 


Kwanini ilikuwa Yerusalemu? Ndipo kulipokuwa na hekalu la Bwana kwa wakati ule, mji Mtakatifu wa Mungu. Lakini Yesu anasema walivunje hekalu la Yerusalemu, Yeye atalisimamisha kwa siku tatu (Yohana 2:19). Nao ndiyo ukombozi halisi na kweli aliyotuletea Kristo kwa njia ya msalaba. Alidharauliwa na kuteswa kwa ajili yetu, akadharau aibu na kustahimili msalaba kwa sababu ya furaha kubwa iliyowekwa mbele yake ili ili atuletee ule wokovu (Ebr 12:2)


Basi leo tambua kwamba Yesu alipokufa alianza ujenzi na alipofufuka alikamilisha ujenzi wa hekalu yaani sisi, maana ndipo Baba atakapojipatia waabuduo awatakao.


6 Hiki ndicho kizazi cha wamfuatao, wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. Zaburi 24:6


Mpendwa nataka uelewa kwamba unayo nafasi ya kupanda mlima aliousema Daudi, unayo nafasi ya kuwa kizazi cha wamtafutao Mungu wa Yakobo. Muandalie Bwana hekalu halisi, mahali ambapo Roho wa Bwana atashuka kusema na wewe, na hapo ndipo Mungu ataikamilisha madhabau yako. 


Mungu wetu haabudiwi tena kupitia siasa na propaganda za wachungaji, mapadri au maaskofu, hataabudiwa katika miti na milima tuitazamayo, wala mapokeo, wala katika majengo yenye picha nyingi za sanamu, bali roho. Kwa kuwa Yeye ni roho. 


Paulo anasema katika Wakorintho


10 Lakini Mungu ametufunulia sisi kwa Roho. Maana Roho huchunguza yote, hata mafumbo ya Mungu.


11 Maana ni nani katika binadamu ayajuaye mambo ya binadamu ila roho ya binadamu iliyo ndani yake? 


12 Lakini sisi hatukuipokea roho ya dunia, bali Roho ya atokaye kwa Mungu makusudi tupate kuyajua tuliyokirimiwa na Mungu. 1 Wakoritho 2:10-12 


Mpendwa nataka ujue leo unamuhitaji Roho wa Mungu ili uweze kumwabudu maana Yeye ni roho hivyo kumwelewa, kumsikia na kumtambua unahitaji  Roho wa Mungu. 


Mpokee leo Bwana Yesu akupe Roho wa Bwana, atakayeongoza maisha yako, atakayekuwa njia yako na kuiweka Yerusalemu ndani yako, hapo ndipo utakapoweza kumwabudu hata ukiwa katikati ya bahari, atakupandisha ule mlima kwa njia ya Roho ambapo Daudi aliusema kwa kila aliyechagua kuwa mzao wa Yakobo ataupanda.


Akianza kukuongoza utaijua kweli maana atakupa nguvu, kiu na shauku ya kusoma na kujifunza neno la Mungu, na hapo utakuwa mtoto wa Mungu, na hapo utamjua Mungu kwa maana utamwabudu unayemjua. Hao ndiyo Baba awataka maana wote waongozwao na Roho hao ndiyo watoto wa Mungu (Rumi 8:14). 


Wapo wakristo wengi leo hawawezi kuabudu bila mchungaji flani, padri fulani, picha au sticker ya nabii wake, hawezi kuomba bila mafuta ya upako, hawezi kusali bila picha ya mtakatifu fulani mbele yake. Nasema bado hujamjua Mungu. Tafuta kumjua Mungu, maana bado huna Roho wa Mungu na huna andiko wala neno ndani yako. 


Bado hujachelewa na Yesu hajafunga mlango wa kukupokea, ikiwa utampokea Yesu leo atakupa uwezo wa kufanyika mwana wa Mungu, atakupa Roho wa Mungu (Yohana 1:12).


Ukiwa upo tayari kumpokea, mpokee Yesu kupitia sala hii ya toba 


Bwana Yesu, ninakuja mbele zako, mimi niliye na dhambi, nakushukuru kwa kazi kubwa ya ukombozi wa dhambi zangu pale msalabani. Leo hii ninakiri Kwamba wewe ni Bwana na mwokozi wa maisha yangu, ninaomba unisamehe dhambi zangu zote na unitakase kwa damu yako ya ushindi. Ninaomba Roho wako ayaongoze maisha yangu siku zote. Amen 


Kapinga Jr 

0718143834 

kapingaemanuel@gmail.com

Blog: sirizabible.blogspot.com

Comments