SIRI ZA BIBLIA: Je, unaweza kupokea Uzima bila Roho Mtakatifu?


Je, tunaweza kupokea uzima bila Roho Mtakatifu?

Jana mtumishi mmoja aliniomba kueleza juu ya Roho  Mtakatifu kwa faida ya wengine. Sikuwa kwenye mazingira rafiki lakini Roho wa Bwana akanisemesha kupitia andiko la 2 Timotheo 3:16, akasema hapo hapo mwanangu utawaeleza na watanielewa. Siri ni hii...


Kama vile ambavyo mtu hawezi kuishi bila maji na chakula ipo hivyo pia kwa kila anayetamani kuitwa Mkristo hawezi kuishi maisha ya kumpendeza Kristo, kumjua Kristo, Kumfunua Kristo na kuenenda katika kusudi la lake bila Roho. Maana Mungu hujifunua kwa walio wake kupitia Roho vinginevyo hutamwelewa.


Kwanini uwe na Roho Mtakatifu? 


Ndiye akupaye kuijua kweli yote kamwe hatutaweza bila Yeye.


Paulo anamwambia Timotheo 


"Kila andiko lenye pumzi ya Mungu lafaa kwa mafundisho..." 2 Tim 3:16a 


Ahaa! Kumbe kila andiko la Mungu ndani yake amesimama Mungu mwenyewe, ambaye ana kweli yote na maarifa yote. Ikiwa Mungu ni roho hapo ndipo unagundua kwamba kumwelewa na kumsikia ni kwa jinsi ya roho tu na si mwili. 


Andiko moja laweza kuwa limebeba maelfu ya mafundisho, yategemea na mafunuo yatokayo kwa Roho, kuna siri nyingi za Mungu katika kila andiko. Lakini hauwezi kufahamu mambo hayo kwa hekima ya dunia hii bali kwa Roho wa Bwana.


Nikwambie ukweli sikuwahi kufundisha au kumwelekeza yeyote kuhusu Roho Mtakatifu kupitia andiko la 2 Timotheo 3:16, ikiwa hata juzi nilisoma hilo andiko lakini sikupata hili funuo, ila leo Roho amenisemesha na kunionyesha Siri ya fundisho la Mungu iliyojificha hapo. Hii ndiyo maana ya kuwa na Roho Mtakatifu anakuwa mwalimu kwako muda wowote na wakati wowote ule kwako.


Ukisoma Wakorintho, maandiko yanaeleza, Roho ndiye ambaye hutufunulia yote hata mafumbo ya Mungu. Kama vile mtu asivyoweza kujua awazacho mwingine kwenye roho yake ndivyo ilivyo ni ngumu kuelewa mafumbo ya Mungu ukiwa huna daraja la kuwaunganisha yaani Roho. Soma 1 Kor 2:10-12 


"Lakini yeye atakapokuja huyo Roho wa kweli, atawaongoza awatie kwenye kweli yote." Yohana 16:13


Maana uijuapo kweli nawe umepokea uzima, ukiwa na Roho utajua kutengenisha mafuta na maji hasa nyakati hizi ambazo zimejaa mafundisho ya uongo yatokayo kwa hao wajiitao watumishi wa Mungu, na wengine mitume na manabii ambao kamwe kweli haimo ndani yao.


"'Yesu akamwambia, mimi ndimi njia, kweli na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi." Yohana 14:6 


Huwezi kumwelewa Mungu, na kamwe hataweza kujifunua kwako kama huna Roho. Kazi kubwa ya Roho ni kumfunua huyu Yesu tupate kumjua. Ukimjua Yesu umepokea ushindi. 


Kazi kwako Pentekoste hii, mpokee Yesu ili ujazwe


Maana kumpokea Roho wa Mungu kuna sharti. Na sharti lenyewe lipo Yohana 1:12, na katika Rumi 8:14 Paulo anakazia, kazi kwako mpendwa.


Kapinga Jr 

0718143834 

kapingaemanuel@gmail.com

Comments

  1. Ukombozi ni sasa na upo karibu kweli kweli, watu yawapasa waelewe neno, tubuni tuwe watoto wa MUNGU.

    ReplyDelete

Post a Comment