USIPOJENGA UKUTA IMARA, SHETANI ATAKUCHEZESHA ATAKAVYO



1 Basi ikawa, walipoarifiwa Sanbalati,  na Tobia na Geshemu, Mwarabu na adui zetu wengine, kwamba nimeujenga ukuta wala hayakusalia mavunjiko ndani yake;... Nehemia 6:1 


Ilikuwa ni kazi ngumu kwa Nehemia kuujenga ukuta, pamoja na vikwazo vingi alivyokutana navyo, lakini alikuwa imara sana, pamoja na kuzungukwa na maadui waliomdhihaki lakini Nehemia aliujenga ukuta, maandiko yanasema hayakusalia mavunjiko ndani yake. Na ndipo walipoanza njama za kumuua. 


Neno "mavunjiko", ukienda kwenye kiswahili cha kisasa katika Biblia Habari Njema (BHN), limetumika neno mapengo maana yake ni mianya. Na mianya ndiyo shetani anaifurahia apate kukutoa kwenye wokovu, nafasi na kusudi ambalo Mungu ameweka mbele yako. 


Adui hachoki, kama vile ambavyo yeye ameijua hatma yake ni katika lile ziwa la moto, yupo kazini usiku na mchana kuhakikisha watoto wa Mungu hawafiki katika ule uzima ambao ni ahadi ya kila mmoja amaaminiye jina la Bwana na kuokolewa. 


Mkristo aliyekaa vizuri katika nafasi yake kwa maana ya kudumu katika neno la Mungu, kudumu katika maombi, mwenye kuenenda katika njia za Bwana na kujazwa Roho Mtakatifu anayo vita kubwa safarini. Uwapo katika safari hii unahitajika kuwa askari imara wa Bwana Yesu, ambaye anatakiwa kuujenga ukuta wake  katika neno na kudumu kwenye maombi siku zote. Ili imani yako iwe hai, na nguvu.


Nazo vita zitaibuka katika ndoa yako, inawezekana huduma yako, kazi yako, biashara yako, ndugu zako, rafiki zako, masomo yako lakini lengo la adui ni kupata mwanya wa kuharibu nafasi au nuru uliyonayo kwa Bwana Yesu. 


Kuna watu ndoa zao zikiyumba hukimbilia kwa mashosti kuomba ushauri, mashosti wengine hukushauri ujiongeze na kutafuta mchepuko, ndoa imekosa mtoto kwa miaka miwili amani inatoweka, siri za za chumbani na mumeo unazitangaza huko saluni, umeanza kusimama vizuri na Bwana Yesu kazini migogoro haimaliziki. Huduma yako imekuwa na kuongezeka unakosa unyenyekevu na kujaa kiburi, kuna watumishi wameamshwa vipawa vyao wewe unaweka fitna na chuki, unaanza kutengeneza mpasuko baada ya kuujenga mwili wa Kristo, unaanza kuwananga na kuwasema watumishi wenzako. Hayo ndiyo mavunjiko ambayo adui huyataka ili akutoe katika nafasi au kuishinda imani uliyonayo, akutoe kwa Bwana Yesu na kukingiza dhambini, kule katika ufalme wake wa giza.


Mpendwa hizi ni nyakati ambazo anguko letu litategemea na aina ya ukuta tulioujenga. Ukiwa imara utamshinda atatafuta kwako mapengo ajipenyeze lakini atakosa mianya kwa kuwa imani yako imebaki kwa Bwana, wakati upigwapo na mawimbi wewe upo imara, unasimama na Bwana, umesimama katika kufunga na kuomba, umedumu katika neno wala huangaishwi na injili za miujiza, adui anapoingiza hila zake anakukuta ukiwa imara sana. Anatafuta upenyo katika ukuta wako hauoni. Mungu atusaidie sana. 


Yesu alimwambia Petro


"31  Akasema, Simoni, Simoni, tazama, Shetani amewataka ninyi apate kuwapepeta kama vile ngano;  32 lakini nimekuombea wewe ili imani yako isipungue; nawe utakapoongoka waimarishe ndugu zako. " Luka 22:31 


Yesu alikuwa akimkumbusha Petro, na kumpa jukumu zito la kuwaombea wengine kama Yeye afanyavyo kwake wakati huo atakapokuwa amerejea kwenye ufalme wake. Yesu mwenyewe alijua ya kwamba Shetani yupo kazini nyakati zote  kuhakikisha watoto wa Mungu wanapotea gizani. Ndiyo maana alimuombea Petro ili imani yake isipungue awe imara, awe ule mwamba wenye kusudi la kuinua na kulijenga kanisa la Bwana. Ule mwamba ulio imara usio na mavunjiko ndani yake.


Wakati tulio nao ni wa kujaa neno la Mungu, ni wakukesha na kuomba na kufunga, na kujaa imani. Imani ndiyo ukuta tulionao kumshinda adui imani yetu isipopunguka kwa Bwana kiasi cha kujenga ukuta imara usio na mavunjiko (rohoni) hapo tumeshinda adui. Yesu aliendelea kutukumbusha kuwa


"24  Basi kila asikiaye hayo maneno yangu, na kuyafanya, atafananishwa na mtu mwenye akili, aliyejenga nyumba yake juu ya mwamba; 25

mvua ikanyesha, mafuriko yakaja, pepo zikavuma, zikaipiga nyumba ile, isianguke; kwa maana misingi yake imewekwa juu ya mwamba." 


Mungu akubariki sana mpendwa, endelea kumwinulia Bwana ukuta imara katika imani yako. Omba bila kukoma, na neno la Kristo likajae kwa wingi ndani yako (Kolosai 3:16-17)

Comments