Kitu pekee unachotakiwa kufahamu katika hii dunia ni kwamba, hakuna anayejali kuhusu wewe isipokuwa wewe mwenyewe.
Tumefika mahali tunahitaji ufahamu kuliko vyeti ili kuweza kufanikiwa. Ni ukweli usiofichika, hivi sasa tuna dimbwi kubwa la wasomi wanaotazamia ajira na kuajiriwa kuliko kujiajiri.
Natamani leo tujifunze pamoja kuhusu Daudi mwana wa Yese ambaye alidiriki kujitoa ufahamu alipokuwa amekimbilia Gathi katika nchi ya ufilisti baada ya kumkimbia mfalme Sauli aliyewinda maisha yake.
1 Samweli 21:10-15
10 Basi Daudi akaondoka, akakimbia siku ile, kwa hofu ya Sauli, akamwendea Akishi, mfalme wa Gathi. 11 Nao watumishi wa Akishi wakamwambia, Je! Huyu siye yule Daudi, mfalme wa nchi? Je! Hawakuimbiana habari zake katika ngoma zao, kusema,
Sauli amewaua elfu zake,
Na Daudi makumi elfu yake.
12 Naye Daudi akayatia maneno hayo moyoni mwake, akamwogopa sana Akishi, mfalme wa Gathi. 13 Akaubadilisha mwenendo wake mbele yao, akajifanya mwenye wazimu mikononi mwao, akakunakuna katika mbao za mlango, na kuyaacha mate yake kuanguka juu ya ndevu zake. 14 Ndipo huyo Akishi akawaambia watumishi wake, Angalieni, mnaona ya kuwa mtu huyu ana wazimu; basi, maana yake nini kumleta kwangu? 15 Je! Mimi nina haja ya watu wenye wazimu, hata mmemleta kiumbe huyu ili aoneshe wazimu wake machoni pangu? Je! Huyu ataingia nyumbani mwangu?
Daudi alipofika katika nchi ya wageni, wakagundua ni yeye aliyeua ndugu yao Goliathi, akapambwa kwa nyimbo za sifa mbele ya Sauli. Lakini kwa wakati huo Gathi palikuwa salama kuliko alipotoka akaamua kujitoa ufahamu mbele ya mfalme Akishi kwa kukuna malango ya Gathi na kuachilia udenda kwenye ndevu zake hivyo mfalme aliamua kumpuuza na kumdharau lakini katika ubongo wake Daudi alijua vema nini afanyacho.
Sijui kama unanielewa lakini nadhani utanielewa, nafahamu una elimu kubwa lakini pasipo kujitoa ufahamu katika zama hizi ambazo taifa lina changamoto kubwa ya ajira, tunaweza kuzeeka na kukata tamaa bila mafanikio. Kwa sababu wengi tunatazama vyeti vyetu kuliko kujifunza namna ya kuishi na mtaa. Daudi Daudi alipojifanya chizi ndiyo ilikuwa mbinu yake na silaha ya kuishi na mtaa, vinginevyo angechungulia kifo na ingekuwa kazi bure kumkimbia Sauli.
Daudi alipakwa mafuta akiwa na umri wa miaka 16 kiuhalisia alikuwa mfalme lakini ni mfalme machoni pa Bwana na si wa kuhudumiwa na kuongoza jeshi la Israel kama Sauli, umehitimu chuo kikuu ukiwa na umri wa miaka 23, 24, 25 au kadhalika. Huu ndiyo wakati mwafaka wa kuanza kujitoa ufahamu ili ufike mahali pa heshima na kuwa mfalme kama Daudi.
Nataka nikwambie katikati ya kujitoa ufahamu kuna mambo mengi ya kujifunza kuliko kuweka standards (viwango) ambavyo havitakusaidia. Kujitoa ufahamu maana yake ni kuivaa aibu bila kujali macho ya watu ambayo katikati ya aibu yako itakuletea matokeo chanya ya muda mrefu ndani ya maisha yako.
Amini kuna watu wametoboa walipoamua kuwa chawa tu wa watu fulani, tena wengine tumewashuhudia wamejivua akili zao wazi wazi, ila hawapo tena kwenye level yetu ya maisha. Muhimu lisiwe jambo ambalo litakuweka mbali na uso wa Mungu. Mfano kwa dada kuuza mwili wake au mwanaume kushiriki michezo ya kamali.
Hapa sisemi kwamba ukawe chawa, hapana, ulikuwa ni kama mfano, lakini unaweza kuivua aibu yako kwa kuambatana na wakulima, kwa kujifunza kuendesha bajaji, kwa kuambatana na mafundi ujenzi, wauza chips, madalali, wafugaji wa samaki na kuku, vibarua wa kukoroga zege n.k. nani anajua katika hayo makundi Roho Mtakatifu anaweza kukupa maono na ukafanikiwa pengine ukalisoma game vizuri kuliko kubweteka.
Ikiwa Ibrahimu alipokea malaika kwa ukarimu wake wa kukirimu wageni, unaweza pia kupokea ndoto yako kupitia unyenyekevu ulionao kwa sababu umeidharau aibu na kutazama maisha yako.
Kama Yesu angeitazama aibu yake, leo hii tusingepokea wokovu lakini maandiko yanasema kwa ajili ya furaha kubwa iliyowekwa mbele yake akaidharau aibu ili na sisi tupate kuokoka.
Waebrania 12:2
tukimtazama Yesu, mwenye kuanzisha na mwenye kutimiza imani yetu; ambaye kwa ajili ya furaha iliyowekwa mbele yake aliustahimili msalaba na kuidharau aibu, naye ameketi katika mkono wa kulia wa kiti cha enzi cha Mungu.
Ili na wewe uokoke katika ndoto ya maisha uliyonayo anza kuidharau aibu leo, ingia piga kazi, ukipata kibarua karikoo hata cha 7,000 piga kazi. Maana katikati ya kujifunza wengi ndipo walipoweza kujua namna ya kupata mtaji, na wengine walikuwa vibarua wa kuuza maduka ya simu na sasa wanamiliki maduka yao, na shuhuda tunazo. Huwezi kufika hapo kwa kuamua kulala kitandani. Weka vyeti pembeni, vua aibu yako kama Daudi.
Nani anajua leo? Pengine kujitoa kwako kanisani ndiyo kupata kazi yako. Nani anajua leo pengine kwenda kwako kwenye kibarua cha kufyatua tofali ukiwa na degree yako ya uhasibu ndiyo kupata kazi ya taaluma yako kwenye kiwanda. Nani anajua leo, pengine ulienda kumsaidia fundi kupandisha tofali ukapata connection ya kazi kupitia mwenye nyumba ambaye ni mtu mkubwa kwenye kampuni yake au serikali. Nani anajua katikati ya story ukiwa unaendesha bajaji kuna abiria anaweza kujua kuhusu taaluma yako na kwa jinsi unavyojituma akakupa ajira bora zaidi.
Maisha ya sasa yanahitaji jicho la tatu. Vinginevyo hatutafika pale alipofika mfalme Daudi. Alipakwa mafuta na kutawazwa kuwa mfalme na Bwana akiwa na umri wa miaka 16 lakini alianza kuketi katika kiti cha enzi akiwa na miaka 40. Miaka 24 ya misukosuko, leo nataka ujue maisha siyo rahisi, kufikia ndoto tulizonazo hatuhitaji kulegeza mikono yetu bali kuikaza na kufanya kazi kwa bidii, kwa kutumia ufahamu wetu na kuachana na habari za macho ya watu, kwa sababu hao watu unawaogopa hawakusaidii. Zaidi watakudharau na kukusema na siku ukifa watakuzika kwa huzuni huku wakisikitika lakini wakati wa nguvu zako hawakuwa na msaada.
Ni kipi bora zaidi, udharaulike leo, na uheshimike kesho, au ubaki kuwa mzigo maisha yako yote. Daudi alikubali kudharaulika pale Gathi kwa sababu aliifahamu kesho yake, hivyo alijua ile aibu ni jambo la kupita tu. Kama ilivyopita kwa Daudi itapita hivyo na kwako pia. Kwa maana Mungu ni mwema sana kwa watu wenye saburi.
Jitoe ufahamu, ukafanikiwe, kazi zipo lakini ajira hakuna. Biashara ni nyingi sana lakini hatuwezi kuziongoza ikiwa hatuna ufahamu. Leo ingia mchezoni.
Kapinga Jr
0718143834
kapingaemanuel@gmail.com
Student of Bible Class

Kubwa San hii kaka asante
ReplyDelete