Anasema Mhubiri
Mhubiri 9:11
Nikarudi, na kuona chini ya jua, ya kwamba si wenye mbio washindao katika michezo, wala si walio hodari washindao vitani, wala si wenye hekima wapatao chakula, wala si watu wa ufahamu wapatao mali, wala wenye ustadi wapatao upendeleo; lakini wakati na bahati huwapata wote.
Laiti kama dunia ingekuwa fair, huenda Edibily Lunyamila angelikuwa tajiri kuliko Simon Msuva, kuliko Thomas Ulimwengu, kuliko Mbwana Samatta. Inasikitisha sana ukiyatazama maisha yake, hayafananii na ukubwa wa mpira wake uliyojenga historia ndani na nje ya Tanzania.
Inaaminika hakuna kijana wa sasa mwenye mpira mkubwa kama wake. Lakini maisha yake yamebaki kwenye vitabu na magazeti. Yamebaki kwenye midomo ya wazee wengi waliomshuhudia huko nyuma.
Masikini hakuwa na bahati maana alicheza soka katika nyakati ambazo mpira ulikuwa burudani na si uwekezaji mkubwa machoni mwa watu wengi wa Tanzania. Laiti kama angekutana na wakati huu, pengine tungekuwa tunasema mengine.
Mhubiri anasema kuna wakati unaweza kusoma sana ukawa na hizo degree, masters na PhD lakini zisilete unafuu kwenye maisha yako. Unaweza kuwa mwanamuziki na mtunzi mzuri wa nyimbo lakini usiwike kwa mafanikio.
Kuna wakati maisha hayana huruma kabisa. Hayakumuhurumia hata Steven Gerrard mbele ya Jordan Henderson. Licha ya mpira mkubwa na kiwango bora kwa muda wote aliotumikia Liverpool Gerrard hakuwahi kutwaa ubingwa wa Ligi wa kuu England (EPL). Lakini Henderson ambaye kwake ubora wa Steven Gerrard anaweza kuutwaa ndotoni tu. Amefanikiwa kubeba mataji yote muhimu akiwa nahodha mwenye bahati.
Kuna wakati anaweza kuajiriwa darasa la Saba akawa na take home nzuri mwisho wa mwezi lakini wewe na degree yako ukang'aa sharubu hadi umauti. Kuna wakati unaweza kuwa na kipaji mno lakini mchezaji anayetafuta kiwango kwa mazoezi akakuzidi kila kitu. Ndiyo kwani David Beckham alikuwa na kipaji gani cha kusajiliwa Real Madrid, ni nyota yake kali ilimbeba. Haishangazi leo hii mwenye PhD kuajiriwa na darasa la saba.
Nataka nikwambie, Daudi mwana wa Yese hakuwa na CV ya utawala lakini Mungu alimpa ufalme akiwa na ujuzi wa kuchunga kondoo na mbuzi. Huyu ndiye Mungu hata kama huamini. Ukijiona katika hali ya kupitwa mbio na wale walio chini yako unaweza kumkimbilia yeye akuinue. Kama unajipa moyo havitoki kwake basi hujawahi kusoma maandiko na ukaelewa nguvu na mamlaka aliyonayo.
Maisha yana bahati na wakati, wapo watu hawajasoma lakini wana bahati ya kupokea maisha mazuri, pesa zinamfuata mahali alipo. Umefaulu vizuri degree yako kumbe ni wakati huo imepitwa na wakati, watu wa veta na mafundi ndiyo muda wao wa kupiga maisha.
Maisha yanahitaji alama za nyakati, zijue nyakati na kutafakari. Simama na Mungu akufundishe kutambua nyakati
Mtafute Mungu afungue mlango wa rehema. Maana asipokufungulia hautaweza kufika unapotamani ufike. Kama Mungu aliumba, basi ni yeye anainua, upo wakati uweke degree pembeni na umtazame Yeye ana rehema nyingi atakukisha katika safari yako. Ukiiona degree ina nguvu na umuhimu kuliko yeye anakucha.
Uliwahi kuamini vyote vinatoka kwake?
Warumi 9:16
Basi, kama ni hivyo, si katika uwezo wa yule atakaye, wala wa yule apigaye mbio; bali wa yule arehemuye, yaani, Mungu.
Kutoka 4:11
BWANA akamwambia, Ni nani aliyekifanya kinywa cha mwanadamu? Au ni nani afanyaye mtu kuwa bubu au kiziwi, au mwenye kuona, au kuwa kipofu? Si mimi, BWANA?
Danieli 4:35
na watu wote wanaokaa duniani wamehesabiwa kuwa si kitu, naye hufanya kama atakavyo, katika jeshi la mbinguni, na katika hao wanaokaa duniani; wala hapana awezaye kuuzuia mkono wake, wala kumwuliza, Unafanya nini wewe?
Muombe Mungu akupe rehema, katika yote mema uyatakayo.
Kapinga Jr
0718143834
kapingaemanuel@gmail.com
DSM

Comments
Post a Comment