SIRI ZA BIBLIA: Mlango wa ajabu wenye siri za mafanikio ya kiwango utakacho.

 


Waamuzi 13:3-5

 *Malaika wa BWANA akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa, huzai; lakini utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto wa kiume. 4 Basi sasa, jihadhari, nakuomba, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi; 5 kwani tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti.*


Nilipokuwa chuo kikuu Mhadhiri wetu aliwahi kutuambia, wao walipokuwa chuoni, mwanafunzi mvivu asiyekuwa na muda binafsi wa kujisomea, akiweka huruma nyakati za mitihani kwamba atafeli walikuwa wanamjibu ni kweli atafeli kwa sababu ni mvivu na hajasoma. 


Kuna wakati hatutakiwi kuwafariji wenzetu kwa mambo ambayo hayawezekani. Au kujaribu kuwafariji wengine mahali walipoanguka kwa matatizo ya kujitakia.


Ikiwa unafahamu siri ya kumaliza masomo yako salama ni kuepuka mimba za mapema, utaishi mbali na zinaa. Ikiwa una malengo ya kupata alama za juu kwenye masomo yako basi utasoma kwa bidii sana. 


Siri pekee ya kufikia malengo uliyonayo katika maisha ni kuweka VIWANGO (Standards). Bila viwango hakuna mahali unaweza kufika. 


Leo katika Biblia tumeona namna Samson mmoja kati ya waamuzi wa Israel alivyozaliwa. Malaika aliyekuja na ujumbe wa kuzaliwa kwake aliwaonya  kuhusu malezi ya mtoto atakayezaliwa kwamba hataonya kileo wala kunyolewa nywele zake, ili kufikia vile viwango vya kiroho ambavyo Mungu alitaka huyo Samson awe navyo.


Nataka nikwambie kwamba kuna mahali usipobadilika na kuweka "standards" hautafika unapotaka kufika, hautafanikiwa jinsi unavyotaka ufanikiwe. Mafanikio ambayo unaota utayaona kwa wengine. 


Ili kutunza heshima yako unatakiwa kuwa mbali na umbea na wambea wenyewe, au unafki na wanafki wenyewe, ni heri mtu akutazame unajisikia lakini ulishaweka viwango vya kutunza heshima yako.


Ukiwa unataka kufanikiwa kibiashara, ni lazma uweke standards za kutunza pesa, nidhamu ya matumizi na kujiepusha na anasa ambazo hazina faida. 


Ili uwe na viwango vya kiroho kadhalika unahitajika kuwa na "standards" za kiroho, ni lazma kuna vitu uviache kama ulevi, zinaa, na kutunza uaminifu wako kwa Mungu, kuwa na muda mwingi wa kuomba na kusoma neno la Mungu. 


Viwango vinaumiza lakini hakuna budi kusimama katika hivyo viwango. Ikiwa ni 


> Bidhaa inahitaji viwango 


> Ikiwa ni huduma inahitaji viwango 


> Ikiwa ni Biashara n.k 


Uliwahi kukutana na mchaga? Anaanza na genge, kisha linakuwa duka kubwa, alafu biashara kubwa sana na baadae anakuwa tajiri kwa sababu wengi wanaweka viwango wakiwa kwenye hali ya kujitafuta. 


Kama unahitaji nyumba weka viwango, kama unahitaji biashara kubwa weka viwango, kama unahitaji mafanikio ya aina yoyote ile ni muhimu kuweka viwango. 


Kuna wanawake wengi siku za leo huenda kukanyaga mafuta ili wapate ndoa, lakini wanasahau kwamba ana mdomo mchafu, ana tamaa mno, ana sifa ya kuomba ovyo, hajui hata kusema hapana. Hata kumshawishi mwanaume avutiwe kuingia na wewe kwenye maisha ya ndoa kunahitaji viwango.


Viwango alivyowekewa Samsoni ndivyo hivyo vilivyomuwezesha kupokea nguvu ya kuwapiga wafilisti wengi zaidi na kunyanyua lile lango zito la mji. Unasubiri nini kuweka viwango vya mafanikio yako. 


Kapinga Jr 

0718143834 

Kapingaemanuel@gmail.com 

DSM

Comments

Post a Comment