"Eliya alikuwa mwanadamu mwenye tabia moja na sisi, akaomba kwa bidii mvua isinyeshe, na mvua haikunyesha juu ya nchi kwa muda wa miaka mitatu na miezi 6." Yakobo 5:17
Matajiri wakubwa duniani kama Elon Musk, Jeff Bezos, Bill Gates, Mukesh Ambani, Aliko Dangote, Bakhresa, Dewji na wengine wengi wana tabia moja na sisi. Wote wanaweza kuumwa, kuhisi njaa, kupata usingizi, kwenda chooni ,kutembea na kukimbia kama sisi, kuchoka na tabia zote za wanadamu.
Leo tunajifunza kupitia Nabii Eliya, ndiye nabii pekee aliyeweza kuzuia mvua isinyeshe kwa miaka mitatu na nusu nalo anga likamtii. Kwanini aliweza? Yakobo anasema ni kwa sababu aliomba kwa bidii. Lakini ni mwanadamu mwenye tabia yetu kwa maana ya sifa za uanadamu.
Yakobo anatufunulia kwamba "BIDII" ndiyo siri pekee iliyoweza kumtofautisha Eliya na wengine. Alikuwa na bidii ya kuomba kiasi kwamba hata mbingu zikamtii kwa neema ya Mungu.
Hakuna siri nyingine katika mafanikio zaidi ya bidii. Bidii kwa upana wake imebeba mengi ndani yake. Bidii siyo kubeba mawe mengi asubuhi hadi jioni bali ni kubeba kwa akili na manufaa.
Kuna bidii ya akili, huko ni kushughulisha akili yako ipasavyo. Ipo bidii ya kutafuta fursa na kutumia vizuri, ipo bidii ya kutunza pesa na bidii ya kutunza nidhamu ya matumizi, ipo bidii ya kutafuta masoko usiku na mchana. Bidii ya kutafuta washirika sahihi katika huduma, bidhaa au kazi zako.
Hakuna uchawi ndugu yangu ni kuweka bidii. Bidii ya kutunza muda na kutumia muda ipasavyo, hili ni eneo ambalo waafrika wengi tumeshindwa, na tumejikuta tukirudi nyuma na kushindwa kufanikiwa. Bidii ya kujizuia hasa vijana wakipata hata 50,000 anawaza kumwagilia moyo na kuwekeza kwenye ngono.
Suleimani katika Mithali 29:18 anasema, "Pasipo maono watu huacha kujizuia." Maana yake ukiwa na maono makubwa
Utatunza afya yako na kujilinda dhidi ya magonjwa.
Utajizuia kushika mimba au kuwa na watoto kabla ya wakati ili kutumiza malengo yako.
Utaheshimu na kutunza kila pesa, ili kufanikiwa kwenye kile ulichoanzisha.
Utajiepusha na dhambi ili kupokea nguvu za Mungu na hapo ndipo huduma yako itanuka.
Unatamani kuwa Mhubiri mkubwa, weka bidii ya kutunza agano kwa Mungu wako, weka bidii katika kufunga na kuomba hapo utakutana na nguvu za Mungu. Unataka kuziona Ahadi za Mungu kwako zinatimia weka bidii ya kusimama katika ukamilifu.
Utalaumu watu bure kwamba wamejiunga na vyama vya wachawi. Lakini shida ni wewe kwa sababu umepiga teke funguo ya mafanikio. Weka bidii kwenye kila jambo. Bila kusahau bidii ya hatua zako. Safari ya mafanikio unayo wewe mwenyewe.
Kwa maana Mungu hutenda na wale walio na bidii, kwa sababu ya bidii alisema na Elisha akatimiza takwa lake. Yupo tayari kusema na wewe leo kama utaweka bidii katika mambo yako yote.
Kapinga Jr
0718143834
kapingaemanuel@gmail.com

Comments
Post a Comment