2 Wafalme 4:2-4
[2]Elisha akamwambia, Nikufanyie nini? Niambie; una kitu gani nyumbani? Akasema, Mimi mjakazi wako sina kitu nyumbani, ila chupa ya mafuta.
[3]Akasema, Nenda, ukatake vyombo huko nje kwa jirani zako wote, vyombo vitupu; wala usitake vichache.
[4]Kisha uingie ndani, ukajifungie mlango wewe na wanao, ukavimiminie mafuta vyombo vile vyote; navyo vilivyojaa ukavitenge.
Basi ashukuriwe Mungu wa BWANA yetu YESU Kristo ambaye leo kwa neema yake ametuongoza tena kuliona juma la Pentekoste mwaka huu.
Leo tunakutana na habari ya mama mjane, ambaye alihitaji msaada kwa Elisha. Alipoulizwa juu ya kile alichonacho, kilichosalia kwake ni chupa ndogo ya mafuta.
Tangu zamani Mungu aliwainua manabii, makuhani na wafalme kwa kuwapaka mafuta. Nayo mafuta yalikuwa ni ishara/utambulisho wa Roho Mtakatifu ambaye huweka nguvu juu ya yote yapate kutendeka.
Ilikuwa rahisi kwa Elisha kugundua kwamba kilichopatikana kwa mama mjane ilikuwa ni ishara ya nguvu za Mungu, alichohitaji ni vyombo vitupu ili sasa nguvu ya MUNGU ianze kutenda kazi ya kuvijaza vyombo vilivyokuwa vitupu.
Ufunuo huu ulianzia wapi? Ngoja tuone
Mwanzo 1:2-3
[2]Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji.
[3]Mungu akasema, Iwe nuru; ikawa nuru.
Kumbe nchi ilipokuwa tupu tena ukiwa na ndipo Roho ya MUNGU ilipoanza kutenda na kuumba. Nataka nikwambie siku ya leo yupo Roho anayetamani kukujaza, lakini hakuna utupu ndani yako kama vile vyombo alivyokusanya mama mjane. Hakuna utupu ndani yako kama ile nchi ambayo mwanzo ilitengenezwa na Mungu mwenyewe.
Fikiria unataka kuweka mboga kwenye sahani iliyo safi wewe unakuta ugali ndani yake. Utaweza kuweka?
Unataka kuweka wali juu ya sahani unakutana na uchafu juu yake. Utaweza kuweka?
Unatamani kuloweka nguo nyeupe ndani ya beseni, unakutana na maji yenye rangi ya udongo. Utaloweka?
Hivi ndivyo Roho Mtakatifu anavyokutana na hali ya miili yetu yaani hakuna utupu ili amimine nguvu zake aanze kutufanya kwa upya kwa kadiri vile apendavyo, ili tupokee nguvu na tuone utendaji wake.
Akifika anakutana na uongo umejaa, kumejaa umbea, unafiki, uzinzi, masengenyo, hirizi, uchawi, ibada za miungu na mambo mengi ambayo ni chukizo mbele za MUNGU.
Elisha hakuhitaji vyombo vilivyojaa bali vitupu, ndivyo Mungu alivyofanya alianza kuumba nchi iliyokuwa tupu. bila kuwa tupu hatuwezi kupokea nguvu na vipawa vya Roho Mtakatifu.
Kubali kuwa mtupu siku ya leo anapopita Roho wa MUNGU apate kukujaza, apate kukutia nguvu, apate kukupa hiyo hekima, apate kuachilia nguvu ya kutambua vipawa na karama ndani yako. Akufanye upya, ukawe mpya.
Kadiri unavyokuwa mtupu (msafi) ndiyo unavyozidi kujaa.
2 Wafalme 4:6
[6]Ikawa, vilipokwisha kujaa vile vyombo, akamwambia mwanawe, Niletee tena chombo. Akamwambia, Hakuna tena chombo. Mafuta yakakoma.
Umebarikiwa.
The Living Gospel (Injili INAYOISHI)
Student of Bible;
Emanuel Saulo (KapingaJr)
0718143834,
Makabe-DSM

Comments
Post a Comment